Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 12:49 am

NEWS: MBUNGE SHANGAZI AISHAURI SERIKALI KUWEKA MFUMO WA UKUSANYAJI MAPATO TPA.

BUNGENI: Mbunge wa Mlalo Rashid Shangazi ameishauri serikali kuweka mfumo wa ukusanyaji wa mapato mzuri katika Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) ili kuweza kupata mapato yanayokusudiwa.




Aidha upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA)ameishauri serikali kuweka msukumo katika mahakama za kikodi ziweze kufanya kazi kwa wakati na zifanye maamuzi stahiki ili kiasi cha shilingi bilioni 84.6 ambacho hakijafanyiwa maamuzi yoyote kiweze kufanyiwa maamuzi.




Ushauri huo ameutoa mei 22 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia taarifa ya kamati kudumu ya bunge ya hesabu za serikali(PAC) kuhusu taarifa za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali(CAG) zilizokaguliwa za serikali kuu na mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha unaoshia mwezi juni 2020.




“Mfumo wa ukusanyaji wa mapato tumeona haupo vizuri,sasa naliomba bunge liielekeze serikali ihakikishe eneo hili la kusimika mifumo linachukuliwa kwa uzito zaidi ili kupata mapato tunayokusudia,”alisema .




Akizungumzia kuhusu TRA amesema pamoja na jitihada kubwa zinaonekana kufanyika bado kuna maeneo yanahitaji maboresho.




“Eneo mojawapo aliloliona CAG ni mashauri mengi ya kikodi hayaamuliwi kwa wakati,takribani bilioni 84.6 hazijafanyiwa maamuzi yoyote ,ukichunguza ni sababu ya mifumo haifanyi kazi kwa haraka na ufanisi,naiomba wizara ya fedha na mipango iweke msukumo katika mahakama za kikodi zifanye kazi kwa wakati,”alisema.



Ushauri mwingine ameutoa kwenye shamba la uwekezaji la miwa la Mkunazi na Mbigili na kuiomba bunge liiazimie bunge litekeleze ahadi yake ya kununua mitambo katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 ili dhamira ya kiwanda hicho la kuzalisha sukari kwa wingi na kupunguza uhaba wa sukari liweze kufanikiwa.




“Uwekezaji huu ni mzuri ili kuziba gape la sukari nchini,lakini bado hatujafikia dhamira hiyo, wamefikia hatua ya kuvuna lakini mpaka sasa mashine haijanunuliwa hivyo wameamua kuuza miwa kwa bei ndogo ili angalau kupunguza hasara,sasa hili sio lengo la kuanzishwa kwa viwanda hivi,”aliongeza Shangazi.