Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 5:33 pm

NEWS: MBUNGE ATAKA BUNGE KUHAIRISHWA KWA KUPANDA BEI ZA VITU NCHINI

Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amelitaka bunge la Jamhuri kuhairisha shughuli zake ili wabunge wa Bunge hilo kjadili kwa undani zaidi juu ya upandaji wa bei za bidhaa nchini kama vyakula na vifaa vya ujenzi.

Akijenga hoja yake mbunge huyo amesema hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza wabunge kuwapa elimu sahihi wananchi wao kuhusu upandaji wa bei za bidhaa muhimu hivyo akaomba bunge lipewe nafasi ya kujadili kwa kina jambo hilo.

Kwa kutumia kanuni ya 54 (1) ambayo inampa nafasi mbunge yeyote kusimama mara baada ya kipindi cha maswali na majibu na akapewa nafasi hiyo kulizungumzia, Gambo amesema wabunge wakijadiliana Jambo hilo itawapa picha nzuri ya nini cha kwenda kusema kwa wananchi wao kuliko ilivyo sasa ambapo bidhaa zinaendelea kupanda lakini hasa zile zinazohusu wananchi moja kwa moja.

Akijibu mwongo huo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson amesema ni kweli kuna tatizo hilo katika maeneo mengi nchini ambapo bidhaa zinazowahusu wananchi wa kawaida zimepanda kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo Spika amesema hoja ya mbunge huyo hajaridhishwa nayo kwa namna ilivyo kwa kutumia kanuni ya 54 (4) kwamba inampa nafasi ya kuagiza kitu gani kifanyike.

“Kutokana na hilo, nakuagiza Kaimu kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni (Dk Dotto Biteko) kwamba jambo hili mlitazame na kufuata utaratibu ambao huwa unatumika katika kusaidia inapotokea bei zinakuwa juu,” ameagiza Spika.

Kwa siku za hivi karibuni bidhaa zimepanda zaidi katika maeneo tofauti nchini ambapo wabunge wameanza kulilalamikia ikiwemo mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma wakitaka Serikali kutafuta namna ya kuokoa hali hiyo kwani kazi ya Serikali ni kulinda watu wake.