Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 8:03 am

NEWS: MBUNGE ALIA NA MAKATO MIKOPO ELIMU YA JUU

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum Ngh'wasi Kamani amesema makato ya mkopo wanayokatwa wanafunzi wanufaika wa elimu ya Juu nchini ya asilimia 15, ni uvunjwaji wa sheria kwa kuwa hakuna utafiti uliofanyika kabla ya kuanza utaratibu huo wa makato.

"Nani alifanya uchunguzi wa kuona vijana wa Tanzania wanaweza kumudu kiasi hicho kwa makato ya asilimia 15 ukijumlisha na makato mengine, je kijana huyu anabaki na kiasi gani," amesema Kamani.

Kamani ameita Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ili kulinusuru kundi hilo ikiwemo kufanya uchunguzi iwapo inafaa kweli mtu kuanza kulipa ndani ya miaka miwili baada ya kuhitimu masomo.

Mbunge huyu ameeleza hayo leo Jumatano Aprili 28, 2021 bungeni mjini Dodoma akibainisha kuwa awali kulikuwa na makato ya asilimia nane ambayo licha ya ugumu wake bado ilikuwa na unafuu kiasi.

Hivi karibuni wadaiwa walilalamika ongezeko la makato ya mkopo kutoka asilimia 8 hadi asilimia 15 kwa mwezi kutoka katika mshahara ghafi wa mdaiwa/mnufaika.

Makato mengine ni tozo ya kutunza thamani ya mkopo ya asilimia 6 (Value retention fee -VRF), tozo ya asilimia moja ya shughuli za kiutalawa (Loan Administration Fee) na adhabu ya asilimia 10 ya deni linalodaiwa kwa anayechelewa kulipa deni baada ya miaka 2 tangu kuhitimu chuo.