Arusha. Kesi ya Uhujumu uchumu na utakatishaji wa pesa inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake 6 imeanza leo hii kwa Shahidi wa nne upande wa Jamhuri, Philemon Kazibila (64) kuiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa, vijana wawili kati ya wanne waliokuwa na mtuhumiwa huyo walijitambulisha kuwa ni maofisa usalama wa Taifa wanaoshughulikia ukusanyaji wa kodi.
Kazibila amedai hayo Jumatatu ya Oktoba 18,2021 mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Patricia Kisinda wakati akitoa ushahidi. Shahidi huyo ambaye ni karani katika kampuni ya Mrosso Injector Pump inayomilikiwa na mfanyabiashara Francis Mrosso, kuwa vijana hao walitangulia kuingia ofisini kwake kumuuliza kama wanalipa kodi kabla ya Sabaya kuingia ofisini humo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Ofmed Mtenga, shahidi huyo alidai kuwa kabla Sabaya na vijana wake kufika ofisini hapo, Januari 22,2021 mmoja wao alikwenda kwenye ofisi hiyo na kupatiwa huduma ambapo alishindwa kupewa risiti kutokana na mashine kutokuwa na mtandao.
Alimtaja mtu huyo aliyefika ofisini hapo siku hiyo Watson Mwahomange na kupewa huduma ya pump.
Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa baada ya Sabaya kufika ofisini hapo alitakiwa kutoka nje ya ofisi hiyo ambapo baada ya muda waliondoka na Mrosso, ambaye baadaye alimpigia simu (Kazibila) na kumtaka ampatie bodaboda kadi ya benki ya CRDB.
Alidai mahakamani hapo kuwa baada ya kumpa dereva huyo kadi ya benki, jioni bosi wake (Mrosso) alirejea akiwa na huzuni na hakujua kitu gani kimemkuta.
Katika hatua nyingine shahidi huyo aliwatambua na kuwashika bega mtuhumiwa wa kwanza (Sabaya) na mtuhumiwa huyo wa tatu kwenye kesi hiyo, Mwahomange, ambapo alidai aliwaona katika eneo hilo.
Katika shauri hilo la uhujumu namba 27,2021 washitakiwa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Kosa la kwanza ambalo ni kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ambalo ni utakatishaji fedha, ambapo washitakiwa wote saba wanadaiwa kujipatia Sh90 milioni huku wakifahamu ni kosa.
Katika shtaka la pili, la tatu na la nne Sabaya peke yake ameshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na rushwa ambapo anadaiwa kuchukua Sh90 milioni na matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Wakili wa Serikali Tumaini Kweka, amemwambia Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Patricia Kisinda, kuwa Jamhuri imeandaa jumla ya mashahidi 20 na vielelezo 16 katika shauri hilo namba 27 linalohusu tuhuma za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha zinazomkabili Sabaya na wenzake.
Washtakiwa wote saba wanadaiwa kujipatia kiasi cha TZS 90M kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso. Imeelezwa mahakamani hapo kuwa Sabaya akiwa na genge lake walienda ofisini kwa Mrosso eneo la Kwa Mrombo jijini Arusha wakiwa na silaha za moto, ambapo walimtuhumu kufanya biashara bila kutoa risiti za EFD, na kudai kuwa mfanyabiashara huyo anaingiza vifaa kutoka nje ya nchi pasipo kufuata taratibu za ulipaji kodi.
Sabaya akiwa na bastola, na John Awenyo akiwa na bunduki aina ya SMG walimtisha Mrosso na kutaka awapatie TZS 100M ili wasimpe kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji pesa.
Mrosso alisema hana kiasi hicho na kuomba awapatie TZS 50M lakini walisisitiza kupewa 100M. Baada ya majadiliano Mrosso alikubali kutoa 90M. Akasindikizwa na vijana wa Sabaya hadi bank akatoa TZS 90M na kumpatia Sabaya.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi saa nane mchana ambapo shahidi wa tano ataanza kutoa ushahidi wake.