- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MAOMBI YA WADHAMINI WA LISSU KUJITOA KUSIKILIZWA JULAI 14
Dar es salaam. MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, inatarajia kuanza kusikiliza maombi ya wadhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu Julai 14 mwaka huu, ambapo wanataka mshtakiwa huyo akamatwe ili wao wajitoe katika udhamini wake.
Kauli hiyo ya mahakama imetolewa jana Juni 17, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba wakati Maombi hayo namba 2/2020 yalikuja wakati upande wa Jamhuri uliomba kuongezewa muda wa kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani.
Lissu ambaye yupo Ughaibuni baada ya kushambuliwa kwa Kupigwa Risasi na watu wasiojulikana mnamo septemba7, 2020 nyumbani kwake Jijini Dodoma.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama iwaongezee muda ili waweze kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani kutokana na maombi yaliyowasilishwa na wadhamini hao.
Hakimu Simba alikubali maombi hayo na kuwapa upande wa Jamhuri muda ambapo wametakiwa ndani ya siku saba wawe wamewasilisha majibu hayo na maombi yatasikilizwa Julai 14.
“Kesi ya msingi namba 208 ya mwaka 2016 itatajwa Julai 14 mwaka huu ikisubiri maombi kusikilizwa na kutolewa uamuzi,” alisema Hakimu Simba.
Februari mwaka huu, wadhamini wa Lissu kwa nyakati tofauti waliieleza mahakama kuwa wamewasilisha maombi mahakamani hapo kuomba itoe hati ya kukamatwa Lissu ili waweze kujitoa udhamini kutokana na mtuhumiwa huyo kutohudhuria katika kesi yake.
Wakili Wankyo alikiri kupokea maombi yaliyoambatanishwa na hati ya kiapo na kuomba mahakama iwape muda wa kutosha waweze kuyachambua.
“Tumepokea hati ya kiapo cha maombi ya wadhamini, tunaomba mahakama itupe muda wa kutosha ili tuweze kuchambua maombi hayo kwa sababu yana vitu vingi,” alidai Wankyo.
Lissu na wenzake wanne katika kesi ya msingi, wanakabiliwa na mashtaka matano, ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Inadaiwa kati ya Januari 12 na 14, 2016 Dar es Salaam, washtakiwa Jabir Idrisa, Simon Mkina na Lissu waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika shtaka la pili, wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mshtakiwa Ismail Mehboob ambaye ni mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la kampuni hiyo lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.