- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MAKAMBA AWATETEA WAKOSOAJI NA WANAO TOA MAONI
Dodoma. Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba amewataka wabunge na watu wanaokosoa au wanaotoa maoni na ushauri wenye nia njema juu ya maswala mbalimbali katika Taifa wasibezwe wala kuhukumiwa kwani kila mmoja dhamira yake iko ndani ya moyo wake.
“Dhamira ya kauli na ushauri na maoni iko ndani ya moyo wa mtu. Atakaposifu kwamba mama Samia (Rais Suluhu Hassan) ameanza vizuri, asihukumiwe kuwa anatafuta cheo. Anapokosoa asionekane kuwa ananongwa, anapokaa kimya isiwe kwamba amesusa. Naomba sana tusihukumiane katika dhamira za kauli,” amesema.
Makamba ametoa maoni hayo hii leo Jumatano Aprili 14, 2021 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Makamba ambaye ni Waziri wa zamani wa Muungano na Mazingira amesema kwa sasa nchi inahitaji umoja na utulivu na kwamba kauli za utengano, kutiliana shaka, kutuhumiana na kuhukumiana hazijengi bali zinawachanganya Watanzania akibainisha kuwa mambo makubwa aliyoyafanya rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli hayatafutika, hayafutwi, hayatapotea na hayatapotezwa kwa kauli yoyote ile ya kubeza.
Amesema kazi aliyoifanya Rais Magufuli anaweza kuichukulia kama fundi aliyeshona nguo nzuri na akitokea mtu akaona kwenye nguo kuna uzi umejitokeza isionekane kuwa ni dhambi.
“Akatokea mtu akasema kwenye hii nguo kifungo kimelegea hebu tukiweke vizuri isionekane kuwa huyu mtu ni msaliti. Na mtu huyo anapokaza kifungo nguo ikapendeza bado sifa ni ya mshonaji,” amesema.
Makamba amebainisha kuwa ametoa kauli hiyo kwa sababu dalili alizoziona sio nzuri na viongozi wanayo haki na wajibu wa kutoa maoni kuhusu mambo yanavyopaswa kwenda.
“Lakini njama, vikundi na vigenge vya kuweka mashinikizo kwamba kipi kifanyike, hatua zipi zichukuliwe si sawa kabisa na haitujengei umoja, uongozi wa nchi ni jukumu kubwa na la kihistoria,” amesema.
Amesema Rais wa nchi ana madaraka na nguvu kubwa na kwa vyovyote vile katika uongozi wake anaacha alama.
Katika uchambuzi wa utendaji wa marais, Makamba amesema rais wa awamu ya kwanza, Hayati Julius Nyerere na waliofuatia hadi Magufuli wameacha alama na ndio asili ya jukumu kulinda yote ambayo viongozi wameyafanya.