Dar es salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua hukumu ya kesi ya uchochezi iiyokuwa ikiwakabili viongozi 8 wa chama kikuu cha Upinzani nchini cha Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kuamuru wahanga hao warejeshewe fedha zao kiasi cha TSh. Mil. 350 ambazo walilipa kama faini.
Uamuzi huo umetolewa hii leo na Jaji Irvin Mgeta ambapo Mbowe na wenzake 7 walihukumiwa Mahakama ya Kisutu March 10, 2020 kulipa faini ya shilingi milioni 350.
Mbowe na wenzake walihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwenye makosa 12 ikiwemo la kufanya maandamano bila kibali na kusababisha vurugu.
Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo walikuwa ni Esther Matiko, Mchungaji Peter Msigwa, Salum Mwalimu, John Mnyika, Halima Mdee, John Heche, Ester Bulaya na Dk Vicent Mashinji.
Hukumu hiyo iliyochukua takribani saa 4, kuanzia saa 7 mchana hadi saa 11 jioni, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kusikiliza ushahidi wa Mashahidi 23 baina ya utetezi na Serikali.
NINI MTAZAMO KWENYE HUKUMU HIYO.
Viongozi wa upinzani wamekuwa wakipita kwenye tanuri la moto tangu kuingia kwa Serekali ya awamu ya tano ambayo ilikuwa ikiongozwa na Rais John Pombe Magufuli ambaye kwa sasa ni marehemu.
Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hukumu hiyo ya Kina Mbowe na wenzake imefungua milango ya kujua kuwa Serekali ya Mama Samia Suluhu Hassan inataka kutenda haki kwa matendo.
Dr. Raurent Mchamna Ngimwa ni Mhadhiri kwenye mmoja ya chuo kikuu hapa nchini anasema kuwa "sisi tunaona na kila mtu anaona mama anafanya kwa matendo, anachofanya Rais Samia ni Kurekebisha baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayaendi sawa, kwa mfano hukumu ya leo (Mbowe na Wenzake) inaonesha kabisa kuwa mama anataka mambo yaende sawa kwa kuwa na taifa lenye kutenda haki, Uhuru na Demokrasia" kwa alivyoanza, sina mashaka sana atamaliza vizuri.
Juni 15 mwaka huu Mkurugenzi wa Mashtaka Sylvester Mwakitalu amesema kuwa aliwafutia mashtaka viongozi wote wa jumuiya ya Uamsho na kutoka gerezani.
Viongozi hao ambao walikuwa gerezani tangu mwaka 2014 kutokana na kukabiliwa na mashtaka hayo ambayo hayana dhamana aliachiwa huru tangu Jumanne Juni 15, 2021 baada ya muendesha mashtaka kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha sheria ya kuzuia ugaidi ya 2002 Januari 2013 na Juni 2014.