Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 9:11 pm

NEWS: MADIWANI WAIBANA HALMASHAURI

DODOMA: Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma limeitaka Halmashauri hiyo kuingiza mara moja TSh Mil 50 kwenye mfuko wa Elimu Ili kutimiza utaratibu walioupitisha ndani ya kikao wa kuwa na mfuko utakaowasaidia wanafunzi wasiojiweza ambao wamefaulu kuendelea na masomo ya sekondari.

Akizungumza katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa bajeti 2020/2021 na mapitio ya nusu mwaka2020/2021 kilichofanyika wilayani humo,Mwenyekiti wa Halmashauri Donald Mejitii ambaye pia ni diwani wa Kata ya Lamaiti amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya mfuko huo kuwa na Sh Milioni 10 tu hadi sasa.

Ameendelea kwa kusema mfuko huo ulianzishwa kwa dhamira njema lengo ikiwa ni kuwasaidia mahitaji wanafunzi wanaofaulu na hawana uwezo,na kuongeza ili kulifanikisha hili tuliamua kwenye baraza kuongeza ushuru wa ng'ombe kutoka Sh 2,000 hadi 4,000 ili nyongeza hiyo iingie kwenye mfuko lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua.

Diwani wa Kata ya Ibugule Blandina Magawa amesema ucheleweshaji wa fedha katika mfuko huo kunapelekea wanafunzi kushindwa kuripoti shuleni kwa wakati kutokana na kukosa mahitaji ya msingi kama sare za shule, madaftari,viatu na pesa za kujikimu kwa wanafunzi waliochaguliwa shule za bweni.

Amesema Fedha hizo siyo Hisani ni fedha ambazo Wananchi wenyewe wanachangia Kama ushuru wakiamini zitakuja kuwasaidia watoto wao sasa kusuasua kwa utekelezaji wake si sawa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Afya na Maji Sostenes Mpandu amesema dhamira njema ya serikali ya kujenga madarasa,kuajiri walimu haitaweza kuleta matokeo chanya kama watashindwa kuendeleza utaratibu ambao wao wenyewe wameuweka.

Akizungumza baada ya kupokea hoja hizo,Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Athumani Masasi ameahidi hadi mwezi wa tatu kiasi hicho cha fedha kitakuwa kwenye akaunti ya mfuko na watoto wote Na wanufaika watapata mahitaji yao.

Akihitimisha hoja hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda amesisitiza fedha hizo zitolewe haraka ili watoto waende shule.


Amesema kutokana Na Fedha hizo kuchelewa kumepelekea mahudhurio duni kwa Watoto mpaka sasa wanafunzi zaidi ya 1000 hawajaripoti shuleni ikimo moja ya sababu kwa wazazi kukosa mahitaji hayo.