Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 10:06 pm

NEWS: MAALIM SEIF AHOFIA ZANZIBAR KUTOBAKI SALAMA BAADA YA UCHAGUZI

Mwenyekiti wa Chama cha upinzani ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kwa inavyoonekana kwa mazigira yaliyopo sasa hivi visiwani Zanzibar uchaguzi hauwezi kuiacha nchi salama.

“Kwa bahati mbaya, ikiwa imesalia miezi miwili tu kuelekea kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu, mazingira ya kisiasa nchini hayatoi taswira ya uchaguzi unaoweza kuiacha nchi yetu salama,” alisema Maalim Seif

Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Maalim Seif alisema duniani kote kipindi cha Uchaguzi Mkuu ni kipindi cha kipekee cha kuamua kuijenga nchi au kuibomoa na kwamba ni vyema Serikali iheshimu umuhimu wa kusimamia uchaguzi huru na wa haki.

Alisema chama chake kimeainisha vikwazo 10 vinavyokwamisha uchaguzi huru na wa haki na kuiomba Serikali kuviondoa.

“Uchaguzi unaoiacha nchi salama na tulivu ni lazima ufanyike kwenye mazingira ya haki, uhuru, na uwazi. Kinyume chake, chaguzi huzaa uhasama, chuki na machafuko katika taifa. ACT Wazalendo tunapenda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 uwe wa kuijenga badala ya kuibomoa Tanzania.

“Tunahitaji kuwa na uchaguzi utakaowaacha Watanzania wakiwa na furaha na matumaini baada ya kutekeleza haki na wajibu wao wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi wanaowataka.

Akitaja vikwazo alivyoeleza kuwa vinakwamisha uchaguzi huru na wa haki, Maalim Seif alidai cha kwanza ni kutokuwapo kwa tume huru za uchaguzi kwa kuwa kwa muundo wake, tume zote mbili, yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), zinaonekana kuwa ni tume za rais badala ya kuwa tume huru za uchaguzi.

Alisema mwenyekiti na mkurugenzi wa NEC na ZEC wanateuliwa na rais (Rais wa Muungano na wa Zanzibar), ambao pia ni Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar na katika ngazi ya halmashauri, wasimamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi ambao kwa asilimia kubwa sana ni makada wa CCM.

Maalim Seif alisema kikwazo cha pili ni hujuma katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba Serikali haijayafanyia kazi mapendekezo ya wapinzani ya kuufuta uchaguzi huo wa mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba mwaka jana.

Alidai kuwa uchaguzi huo umesababisha kuwepo kwa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji ambao hawana uhalali wa kisheria wala wa kisiasa, kwa sababu hawakuchaguliwa na wananchi.

“Kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu, ni wakati mwafaka kwa mamlaka zinazohusika kutathmini kosa hilo la kihistoria,” alisema Maalim Seif.

Alitaja kikwazo cha tatu ni hujuma kwenye uandikishwaji wapigakura Zanzibar.

Alidai kuwa uandikishwaji umetawaliwa na hujuma za makusudi zenye lengo la kuhakikisha kuwa maelfu ya wananchi wananyimwa haki yao ya msingi ya kupiga kura.

“Kikwazo cha nne ni hujuma kwenye ugawaji wa majimbo Zanzibar… ZEC imetangaza kupitia upya idadi na mipaka ya majimbo ya uchaguzi baada ya kuongeza majimbo mwaka 2015 kutoka 50 na kuwa 54.

“Sasa wamepanga kukata upya majimbo ili kuisaidia CCM… Taarifa za uhakika za ndani ya ZEC zinaonyesha mipango yake kwa kushirikiana na CCM inalenga kuyapunguza kutoka 54 waliyoyaongeza mwaka 2015 na kurudi 50, lakini katika muundo tofauti na uliokuwepo kabla ya mwaka 2015.

“Ni vipi na kwanini mwaka 2015 waliongeza majimbo manne mapya kisiwani Unguja, lakini leo wanapanga kurudisha majimbo 50, wapunguze majimbo mawili kutoka Pemba ambako hawakuongeza jimbo? Haya yote yanathibitisha njama ovu zinazoratibwa na ZEC katika kuhakikisha kuwa uchaguzi unahujumiwa,” alidai Maalim Seif.