Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 1:28 pm

NEWS: M-PESA KUPATIKANA NCHI 200 DUNIANI

Nairobi. Kampuni ya Safaricom imesaini mkataba na kampuni ya VISA, ili kuwawezesha watumiaji wa M-Pesa kulipia bidhaa na huduma katika nchi zaidi ya 200 duniani, baada ya muungano huo.

Safaricom ilitia saini mkataba huo na kampuni hiyo na kubuni kadi ya M-Pesa GlobalPlay Virtual card, inayowaruhusu wateja kutoa ama kutuma hadi KSh300,000 sawa milioni 6 kwa siku moja.

Mkataba huo umeupandisha hadhi mfumo wa malipo wa M-Pesa kuwa kiwango sawa na majukwaa mengine ya kimataifa ya malipo duniani.

Ili kuingia kwenye mfumo huo, wateja watahitajika kubonyeza *334#, kisha sehemu ‘6’ (Lipa Na M-Pesa).

Baadaye, watabonyeza kidude ‘M-PESA GlobalPay.’

“Kwa kushirikiana na kampuni ya Visa kubuni kadi ya M-Pesa GlobalPay Visa, tunalenga kuwawezesha wateja wetu kutumia njia hii popote walipo duniani,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, Bw Peter Ndegwa.

Kampuni hizo mbili pia zinalenga kuzindua kadi hiyo mpya katika nchi za Tanzania, DRC Congo, Msumbiji, Lesotho na Ghana.

Mkataba huo mpya pia unatarajiwa kuisaidia kampuni ya Visa kupenya kwenye soko la Afrika.

“Visa imejitolea kupanua mfumo wa malipo yake kote barani Afrika kwa kufungua soko la dunia nzima ili kumfaa kila mteja. Ushirikiano huu mpya na kampuni ya Safaricom ni hatua kubwa katika kutimiza lengo hilo,” akasema Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ukanda wa Afrika Mashariki, Corine Mbiaketcha.

Mkataba huo pia unatarajiwa kupiga jeki mapato ya Safaricom kupitia M-Pesa, hasa baada ya mapato ya mfumo huo kushuka kwa mara ya kwanza nchini kwa muda wa miaka mitano iliyopita.

Mwaka uliopita, Safaricom ilipata mapato ya Sh82.6 bilioni kupitia M-Pesa, ikilinganishwa na mwaka 2020, ilipojipatia mapato ya Sh84.5 bilioni.

Kiwastani, Safaricom imekuwa ikipata faida ya Sh8 bilioni kila mwaka kupitia M-Pesa tangu 2018.

Safaricom imekuwa ikiweka mikakati kuboresha mfumo wa malipo kupitia njia ya kidijitali tangu 2020, baada ya watu wengi kuegemea utumaji pesa kupitia njia hiyo.