Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 6:45 pm

NEWS: LISSU KUREJEA NCHINI JULAI 28 MWAKA HUU

Kaimu Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA Tundu Lissu amesema anatarajia kurudi nchini humo Julai 28.mwaka huu.

Mwanasiasa huyo kwa sasa yuko ughaibuni ambapo alienda kupata matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017.

Akizungumza jana katika mkutano unaoendelea kwa njia ya mtandao ulioandaliwa na taasisi ya The Resistance Bureau, Lissu amesema ameshakata tiketi ya ndege na watanzania watarajie kumpokea Julai 28.

Lissu ametangaza niya ya Kugombea Urais katika uchaguzi ujayo kupitia chama chake cha Chadema.

Mjadala huo umewahusisha viongozi kadhaa wa upinzani na wanaharakati mbalimbali wa Afrika, washiriki wa Afrika Mashariki wakiwa Bobi Wine mpinzani kutoka nchini Uganda na Tundu Lissu wa Tanzania

Akijibu swali kuhusu kama anahofu kuwa anaweza kuzuiwa kuingia nchini mwake, Lisu amesema: ''Sina sababu ya kuamini kuwa nitazuiwa kurudi nyumbani, mimi si mhalifu niliondoka nje ya Tanzania nikiwa sina fahamu, nilishambuliwa kwa risasi mara 16 na watu ambao mpaka sasa hawajakamatwa.''

''Hivyo ninarejea nyumbani kuikabili serikali iliyosema kuwa haina hatia katika tukio hilo la jaribio la kuniua, kunizuia kutadhihirishia dunia kuwa ilihusika na shambulio la mwaka 2017 kama nilivyosema sina sababu ya kuamini kuwa nitazuiwa kurejea nyumbani''. Alieleza Lissu kwenye mkutano huo.

Juma lililopita Lissu aliwakilishwa na Wakala wake David Djumbe kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama cha CHADEMA kuwania nafasi ya urais.