Home | Terms & Conditions | Help

April 4, 2025, 7:32 am

NEWS: KISHINDO CHA MTATURU JIMBONI.

SINGIDA: Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,Julai 12,2022,ameanza ziara ya kijiji kwa kijiji ambapo siku ya kwanza ametembelea kata ya Mang'onyi kutoa mrejesho wa Bajeti ya Mwaka wa fedha 2022/2023,iliyopitishwa na Bunge mwishoni wa mwezi June 2022 jijini Dodoma.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vya Tupendane na Mang’onyi,Mtaturu amesema mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan umeakisi dhamira yake ya dhati Katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Amesema katika ujenzi wa madarasa 15,000 nchi nzima,Wilaya ya Ikungi imepatiwa madarasa 67 yenye thamani ya sh Bilioni 2.6.

“Tumepata Sh Milioni 800 ya kumalizia hospital ya wilaya na Sh Milioni 300 ya kununua vifaa tiba,pia tulipata Sh Bilion 1.5 za kujenga Barabara na mgawanyo wa Sh Milioni 330 kwa ajili ya kufungua Barabara ya Mang'onyi-Ntewa na kujenga madaraja,”amesema.

Aidha amesema Sh Milioni 280 zimetolewa kujenga daraja kubwa maeneo ya Minyinga na kufanyia matengenezo Barabara ya Utaho-Minyinga-Makiungu,Sh Milioni 220 za kujenga daraja na kufungua Barabara ya Siuyu-Nali-Makotea na Sh Milioni 600 ya kufungua na kujenga madaraja,makaravati na Barabara ya Misughaa-Msule-Sambaru.

Mtaturu amesema bajeti iliyopitishwa imelenga kuleta unafuu kwenye maisha ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo kwenye sekta za uzalishaji hususani kilimo.

Amesema pamoja na utekelezaji huo wa miradi ya maendeleo wa mwaka mmoja wa Rais Samia,bajeti iliyoanza Julai Mosi,2022, imesheheni mipango ya utekelezaji kwenye sekta mbalimbali hivyo kuwaomba wananchi kuendelea kumuombea na kumuunga mkono Rais katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo.

“Bajeti imezingatia ahadi zilizopo kwenye Ilani ya uchaguzi kwa kuzingatia vipaumbele kwenye sekta za Elimu, Afya,Miundombinu ya Umeme, Maji,Barabara na huduma za jamii,kwa niaba ya wananchi nimshukuru Rais wetu mpendwa kwa kuridhia fedha za maendeleo kuletwa kwenye Jimbo na wilaya yetu ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,”amesisitiza.

Amesema kwa sasa umeme unaendelea kusambazwa vijiji vya Kimbwi,Mungaa,kinku,Mwisi,Lighwa,Mampando,Ntuntu,Ntewa,Taru,Mbwanjiki na Matongo.

Ametumia mkutano huo kuwahamasisha wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi litakayofanyika Agosti 23,2022 ili serikali iweze kujua idadi halisi ya wananchi na hivyo kuwezesha kupanga mipango yake kwa uhakika.

Ziara hiyo maarufu kama "HUDUMA JIMBONI" itakua kata kwa kata, Kijiji kwa Kijiji na hakika hakuna jiwe ambalo halitageuzwa.

#Huduma jimboni

Singida Mashariki

#SENSA 2022,Jiandae jitokeze kuhesabiwa ewe

Mwana Singida Mashariki.