Home | Terms & Conditions | Help

December 3, 2024, 8:11 pm

NEWS: KINA MDEE KUJIELEZA SABABU ZA KUPINGA KUVULIWA UWANACHAMA

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ya Dar es salaam imeanza kusikiliza sababu za kina Halima Mdee na wenzake 18 kuomba ridhaa ya kufungua kesi kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema, huku mawakili wao wakishusha hoja za kuomba ridhaa hiyo.

Maombi ya kina Mdee yameanza kusikilizwa na Jaji Mustapha Ismail leo Alhamisi Juni 30, 2020 mchana.

Mawakili wa kina Mdee wameanza kubainisha maombi muhimu yanayohitajika katika maombi ya ridhaa kwa mujibu wa sheria na rejea ya hukumu za Mahakama Kuu kuhusiana na suala hilo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa hoja zinazolalamikiwa.

Mambo mengine wamesema kuwa waombaji kuonyesha kuwa na maslahi, muda muafaka wa kufungua maombi hayo, kuonyesha hatua zilizochukuluwa kutafuta haki zinazoombwa kabla ya kwenda mahakamani na kubainisha mdaawa anayelalamikiwa.

Wakili Ipilinga Panya ameieleza mahakama kuwa katika maombi hayo wateja wao kupitia viapo vyao na maelezo yaliyoambatanishwa katika hati ya maombi wamekidhi vigezo hivyo vyote.

Baada ya kuyataja mambo hayo ya msingi yanayopaswa kutimizwa katika maombi hayo, wameanza kuyafafanua moja baada ya lingine kuithibitishia mahakama ni namna gani waombaji wamekidhi matakwa hayo ya kukubaliwa kuruhusiwa kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama

Kuhusu hoja ya waombaji kuwa na maslahi, wakili Panya ameileza mahakama kwamba waombaji katika viapo vyao wameeleza kuwa wao ni wabunge wa viti maalum waliodhaminiwa na Chadema kwa mwaka wa 2020.

Hivyo amedai kuwa pia wameathirika na uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema kuwafukuza uanachama bila kufuata taratibu wala kuwasikiliza.

Kuhusu kigezo cha muda wakili Panya amesema kuwa wamefungua maombi hayo ndani ya muda.

Amefafanua kuwa sheria inaelekeza maombi kama hayo yafunguliwe ndani ya muda wa miezi sita tangu kutolewa kwa uamuzi unaolalamikiwa.

Amefafanua zaidi kuwa uamuzi huo wa Baraza Kuu ulitolewa Mei 11, 2022 na maombi hayo yalifunguliwa Juni 23, 2022.

Kuhusu hoja zinazalamikiwa, Wakili Aliko Mwamanenge amesema kuwa uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama unakiuka misingi ya haki kwa kuwa kwanza ulitolewa upande mmoja na wao hawakupewa haki ya kusikilizwa kuanzia kwenye Kamati Kuu na kwenye Baraza Kuu.

Amesema kuwa hoja hiyo haijapingwa na Chadema katika kiapo chake kinzani badala yake wamedai tu kuwa walipewa hati za wito kwenye Kamati Kuu lakini hawakuitikia.

Pia amesema katika Baraza Kuu, wajumbe waliotoa uamuzi wa upande mmoja kwenye Kamati Kuu ndio haohao waliohusika katika uamuzi wa Baraza Kuu.

Pia wakili Mwamanenge amedai kuwa kumekuwa na msukumo mkubwa kutoka kwa mjibu maombi wa kwanza, Bodi ya Wadhamini Chadema (iliyosajiliwa) kwenda kwa Spika kumtaka aijulishe Tume ya Taifa ya Uchaguzi itangaze kuwa nafasi zao ziko wazi na kwamba ndio maana wakaomba amri ya zuio.

Hivyo amesema kuwa waombaji wamethibitisha kuwepo kwa masuala yanayobishaniwa na wanastahili kupewa ridhaa ya kufungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama.