- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: KESI YA SABAYA BADO KAMBA NGUMU
Arusha. Kesi ya Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne jana imeendelea tena na watuhumiea hao wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa mara nyingine, kwa ajili ya kusikilizwa kwa mashtaka yanayowakabili.
Kwa upande wa shtaka la kwanza la uhujumu uchumi na utakatishaji fedha namba 27 la mwaka 2021 ambalo imesomwa mbele ya hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Martha Mahumbuga, Wakili Mkuu wa Serikali msaidizi Abdalah Chavula ameiomba mahakama kutaja tarehe nyingine kwa ajili ya kulisikiliza kutokana na upelelezi kutokamilika.
Wakili wa utetezi Moses Mauna ameiomba mahakama kuharakisha upelelezi wa shtaka hilo pamoja na kuwapatia hati ya kesi hiyo.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Martha Mahumbuga ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 2 mwaka huu itakaposikilizwa tena kutokana na upelelezi kutokamilika.
Kwenye shtaka la pili ambalo ni la jinai la unyang'anyi wa kutumia silaha lenye makosa mawili linalowahusu watuhumiwa watatu ambao ni Lengai Ole Sabaya, Sylvester Nyegu na Daniel Mbula ambalo limesomwa mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Arusha Salome Mshasha, Wakili wa Serikali Tarcila Gervas ameiambia mahakama kuwa Februari 9 mwaka huu watuhumiwa hao walifika kwenye duka la Saad lililopo mtaa wa Bondeni - Arusha na kuwaamuru Wafanyakazi wa duka hilo kulala chini huku wakiwapiga ngumi, mateke na makofi na kuwanyooshea bunduki wakiwatishia kuwafyatulia risasi.
Katika shtaka hilo mmoja wa watuhumiwa anadaiwa kumfunga kamba diwani wa kata ya Sombetini Bakati Msangi na kuchukua shilingi laki 3 na 90 elfu na simu aina ya Tekno na shilingi elfu 35 kutoka kwa Ramadhan Rashid.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa Watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti na kukiri kuwepo kwenye duka hilo, lakini Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha amewahoji iwapo walitenda tukio hilo ambapo wamekana.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na kesi mbili ambapo kesi ya kwanza namba 27 ya mwaka 2021 ina mashtaka manne na kesi ya pili namba 66 ya mwaka 2021 ina mashtaka mawili.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai mbili mwaka huu itakaposikilizwa tena.