Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 9:54 pm

NEWS: ILANI YA CCM IMETEKELEZWA MAHAMBE.

MAHAMBE SINGIDA: Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro amezindua mradi wa maji katika Kijiji cha Mahambe unaoenda kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu waliyokuwa wanaipata wananchi.

Mradi huo umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 11.5 ambapo Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amechangia Shilingi Milioni 9 na Shilingi Milioni 2.5 ni nguvu za wananchi.

Akizungumza katika uzinduzi huo,mkuu wa wilaya huyo amesema baada ya kuzindua mradi huo wanachofanya kama serikali ni kuongeza idadi ya vituo vya kuchotea maji ili kurahisisha upatikanaji wa maji hayo karibu na wananchi.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametutuma kufanya kazi,na mimi nikishirikiana na Mbunge tunaifanya kazi hiyo,niwahakikishie kuwa tutaongeza vituo vingine vya kuchotea maji ili huduma hii isogee karibu yenu zaidi na hivyo tutekeleze Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),kwa vitendo,”alisema.

Kwa upande wake Mbunge Mtaturu amesema amefarijika kuona kile alichokipigania kimezaa matunda na wananchi sasa wanapata maji.

“Ilikuwa ukifika hapa unapiga maneno lakini wananchi wanakwambia maji,hivyo kutokana na tatizo hilo nilivyofika bungeni tu kwa awamu ya pili kazi yangu ilikuwa ni kuisumbua serikali ili maji yapatikane hapa, nah ii ilikuwa ni kiu yangu kubwa kuona mradi huu unakamilika na wananchi mnapata maji,niwaambie ndugu zangu tukiutumia vizuri mradi huu tutaweza kuongeza vituo vingi zaidi,”alisema Mtaturu.

Ametaja hatua walizochukua hadi kukamilika kwa mradi huo,“Cha kwanza tulichofanya hapa kuna kisima kilichochimbwa na wafadhili tangu mwaka 2013,hivyo kupitia mfuko wa Jimbo tulitoa Sh Milioni 9 ili kuwapatia miundombinu ya maji na hivyo sasa kero hii imeisha,’’Mtaturu.

Mbali na hilo amesema ameweka Tanki la Lita 10,000, mabomba yenye urefu wa mita 770 na vituo viwili vya kuchotea Maji ambapo wananchi nao walitoa nguvu kazi kwa kushiriki uchimbaji wa Mtaro wa kusambaza maji.

Sophia Hamisi Mkazi wa Kijiji hicho ameishukuru serikali na kufananisha uzinduzi huo nimfano wa familia iliyokaa muda mrefu bila ya kupata mtoto na hatimaye Mungu akasikia maombi yao na kuwapatia mtoto.

“Leo tunasherehekea kupata maji,tunafurahi kuona ile tabu tuliyoipata kwa miaka mingi ya kuamka asubuhi kufuata maji sasa imekwisha,tumewahi kuwa na wabunge kwa awamu mbili wanaotoka katika kijiji hiki lakini hatujawahi kuona manufaa,sasa mbunge wetu Mtaturu ameweza kuwasilisha kero yetu ya maji na sasa tuna neemeka na maji safi na salama tunayopata,sasa hatutawaza maji tena bali tutawaza shughuli za kutuongezea kipato,alisema Sophia.

Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025,Ibara ya 100 imeweka bayana lengo la CCM kuwa ni kuona nchi inaendelea kuwa na usalama wa maji na kwamba huduma ya majisafi na salama inaendelea kuimarishwa na kuwafikia zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa Vijijini na asilimia zaidi ya 95 Mijini ifikapo 2025.