Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 8:09 am

NEWS: HOSPITALI YA AGA KHAN YACHUNGUZWA NA JESHI LA POLISI

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeanza kuichunguza Hospitali ya Aga Khan ya Jijini Dar es Salaam, kufuatia kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi mbalimbali kutozwa gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya kupumua.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Kamanda wa Polisi, kanda maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa amesema kuwa jeshi la Polisi limepokea malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya Hospitali ya Aga Khan ya Jijini Dar es Salaam kutoza gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wa matatizo kifua (Pneumonia) ambayo husababisha matatizo ya upumuaji.

Aidha wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali hiyo, pindi wanapofariki dunia kumekuwa na tabia ya kuzuia miili ya marehemu na kudai kiasi kikubwa cha fedha kinyume na maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.

‘’Management ya hospitali hiyo imekuwa na tabia mbaya ya kuzuia miili ya marehemu wanaokuwa wamefariki pale na baada ya kuzuia wanalazimisha kutoa bili kubwa ambayo haiendani na tiba ambayo kimsingi mgonjwa alikuwa anapata’’.

‘’Wamekuwa wakifanya hivi kwa muda mrefu na wakati Fulani kupelekea wahusika kuuza vitu vyao ili kukomboa miili.’’ Alisema kamanda Mambosasa.

Hata hivyo Mambosasa amesema kuwa uchunguzi utakapokamilika na kubaini tuhuma hizi hatua kali za kisheria zitachukuliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto dhidi ya Hospitali hiyo.