Home | Terms & Conditions | Help

January 30, 2025, 11:40 am

News: Hatimaye Janet Jackson Ajifungua akiwa na umri wa miaka 50

NEW YORK: Mwanamuziki mashuhuri nchini Marekani Janet Jackson amejifungua mtoto wa kiume akiwa na umri wa miaka 50, Taarifa kutoka kwenye familia yake imethibitisha.

Taarifa imesema mwanamuziki huyo na mumewe Wissam Al Mana, ambaye ni mfanyabiashara kutoka Qatar, wana furaha kumpata mtoto wa kiume kwa jina Eissa Al Mana.

"Janet alijifungua bila matatizo yoyote na kwa sasa anapumzika," afisa wake amesema.

Watu walianza kushuku kuwa alikuwa ameshika mimba Aprili mwaka jana alipoahirisha ziara yake ya kutumbuiza ya Unbreakable.

Alipakia video kwenye Twitter wakati huo na kuwaambia mashabiki kwamba alikuwa anaahirisha ziara hiyo "kwa sababu kulitokea mabadiliko ya ghafla".

"Nilifikiri ni muhimu sana kwenu kuwa wa kwanza kufahamu hili," alisema, na kuongeza: "Tafadhali, naomba mjaribu kunielewa kwamba ni muhimu sana nilifanye hili kwa sasa."

Alisema alitaka kuangazia kuunga familia na mumewe, ambaye walifunga pingu za maisha mwaka 2012.

Jackson alikuwa awali ameonekana akinunua nguo na vitu vingine vya kutumiwa na watoto London.

Janet Jackson ndiye mtu mashuhuri pekee aliyejifungua mtoto akiwa na umri mkubwa.

Mshindi wa tuzo ya Oscar Halle Berry alijaliwa mtoto wake wa pili akiwa na miaka 47 miaka mitatu iliyopita.

Na mke wa John Travolta, Kelly Preston, alijifungua mtoto wake wa tatu akiwa na miaka 48.

Nchini India hata hivyo, kuna wanawake watatu ambao wamedaiwa kujifungua watoto wakiwa na zaidi ya miaka 70.