Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 1:27 am

NEWS: GWAJIMA AADHIBIWA VIKALI NA BUNGE,

Dodoma. Kamati Maalum ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imemtia hatiani Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima kwa makosa ya utovu wa nidhamu, kuchonganisha mihimili, dharau, na kulidhalilisha bunge , hivyo kamati hiyo imependekeza Mbunge huyo kutohudhuria mikutano miwili au mitatu ya Bunge.

Kamati hiyo pia imeviomba vyombo vya dola vifuatilie vitendo vya Askofu Gwajima na kufafanua kuwa kuna dalili za jinai ndani yake, na kuomba shauri hilo liende pia kwenye vyombo vya utumishi wa umma na chama kwa hatua.

Adhabu hizo zimetolewa kwenye Ripoti ya kamati hiyo iliyowasilishwa leo Agosti 31, 2021 Bungeni jijini Dodoma mara baada ya kumaliza kumuhoji Josephat Gwajima kwa siku mbili tofauti kwa tuhuma za kuzungumza uongo na kulishushia Bunge hadhi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo akisoma taarifa yake amesema Shahidi alikiri kauli zote ni zake 100% na akasema ni mahubiri.

"niliyasema nikiwa Kanisani na ninayasema kama Askofu, kosa kubwa ni kujaribu kuyakosoa mahubiri, huwezi ku-question mahubiri, Kamati ilijiridhisha kuwa mahubiri yanayotolewa yanapaswa kuzingatia Sheria za Nchi hivyo kauli zinazotolewa haziwezi kuwa na kinga ya kuhojiwa”

“Gwajima ni Mbunge na Kiongozi kwa hiyo anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa, tuhuma za kuchonganisha Mhimili wa Bunge na Serikali au Serikali na Wananchi zinajidhihirisha wazi kwenye kauli za Askofu Gwajima”

“Gwajima alishindwa kuthibitisha kauli zake na hana kielelezo chochote kama alivyowaaminisha Wananchi, suala la Viongozi kupewa rushwa hakutoa ushahidi wowote, kamati imemtia hatiani Askofu Gwajima”

“Kuhusu adhabu ya utovu wa nidhamu uliokithiri wa Askofu Gwajima ni kuwa kanuni zinataka asihudhurie mfululizo mikutano miwili au isiyopungua mitatu, Kamati ilishangazwa na vitendo alivyovifanya mbele yake na iliona ni dharau”

“Askofu Gwajima hakukiri wala kujutia makosa yake, alionyesha dharau hivyo Kamati imemtia hatiani, Bunge linaazimia kuwa apewe adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili mfululizo ya Bunge baada ya kupitisha azimio hili” amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maadili Emmanuel Mwakasaka.