Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 3:26 pm

NEWS: DKT BASHIRU AWAKARIBISHA CCM AKINA MDEE NA WENZAKE

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi,(CCM), Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewakaribisha wanawake Wote kutoka vyama vya upinzania waliofukuzwa kwenye vyama vyao ili kujiunga na Chama hicho.

Hivi karibuni kamati kuu ya Chadema iliwafuta uwanachma wabunge 19 wa Viti maalum akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la wanawake Taifa Halima Mdee kwa madai ya kufanya usaliti ndani ya chama hicho.

Uamuzi huo ulitokana na maazimio ya Kamati Kuu iliyokutana siku ya Ijumaa Novemba 27 Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Bashiru ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa Kamati za Jumuiya za Chama hicho uliofanyika leo Novemba 29, 2020 jijini Dodoma ambapo amesema kuwa, vyama vya upinzani vilikuwa na wagombea wengi wanawake majimboni na walikuwa na ushahidi.

“Upinzani walikuwa na wakina Mama wenye ushawishi sana na wametusumbua sana huko majimboni haikuwa rahisi. Lakini nasikitika sana vyama vyao haviwathamini na havitaki kuitambua nguvu yao, Wanawake wa shoka wote wa Upinzani karibuni CCM milango iko wazi”, amesema Dkt. Bashiru.

Akizungumzia suala la ushindi wa Chama, “Hatuna mitambo ya kuiba Kura sisi kama Marekani, sisi mitambo yetu ni mabalozi wetu ambao walifanya kazi Usiku na mchana sababu tulikuwa tunashindana na vyama vilivyoishiwa sera. Vyama vimeshindwa kwa halali vinatafuta sababu kuna Watu wametukana siku 60 za kampeni badala ya kumwaga sera, niwapongeze sana Vijana wa Chama cha Mapinduzi mmeonesha uvumilivu sana kipindi chote cha kampeni”.

Kikao cha kamati kuu ya Chadema kilikuwa kimeitishwa ili kuwajadili wanachama wao walioapishwa Novemba 24 kuwa wabunge wa viti maalum mjini Dodoma.

Hatua hiyo ya kuapishwa ilipingwa na viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho wakieleza kuwa hakikuyapitisha majina yao na kuitaka tume hiyo kusema ukweli.

Walengwa ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Kufuatia kuapishwa kwao, Mnyika alifanya mkutano na wanahabari na kueleza kuwa hakuna kikao kilichokaa na kupitisha majina hayo na kuyapeleka NEC lakini leo tume hiyo imemtaja Mnyika kuwa aliwasilisha majina hayo.

Lakini katika taarifa yake kwa umma, Mahera alisema, “ifahamike kwamba katibu mkuu wa Chadema alimuandikia mkurugenzi wa NEC barua yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/20/TU/05/141 ya Novemba 19 ambayo iliwasilisha orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum.”

“Tume ilitumia orodha iliyowasilishwa na Chadema kuteua wabunge wa viti hivyo. Hivyo, wabunge wanawake wa viti maalum wa Chadema waliteuliwa kwa kuzingatia taratibu zote za kikatiba na kisheria," aliongeza.

Kikao cha Ijumaa ca chama kiliongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kuhudhuria ni makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohammed; katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika naibu wake Zanzibar, Salum Mwalimu huku makamu mwenyekiti bara, Tundu Lissu, aliyekuwa mgombea urais kwa tikiti ya chama hicho, akishiriki kwa njia ya mtandao.

Pamoja na viongozi wa chama, wajumbe wengine wa kikao caha Ijumaa walikuwa ni John Heche, Mchungaji Peter Msigwa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, Boniface Jacob, Suzan Kiwanga, John Mrema, Julius Mwita, Rodrick Rutembeka, Patrick Ole Sosopi, Hashim Juma na John Pambalu, ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza la vijana wa chama hicho.