- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: CUF YASEMA INAKARIBISHA MUUNGANO WA VYAMA UCHAGUZI MKUU
CHAMA cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania, kimejitokeza na kusema kuwa kipo tayari kama chama cha Upinzani nchini kushirikiana na vyama vingine vya upinzani vyenye dhamira ya kweli kukiondoa madarakani Chama Tawala (CCM).
Msimamo huo umetolewa leo tarehe 6 Juni 2020, na Juma Killghai, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, alipokuwa akitoa ratiba ya kuwapigia kura za maoni na uteuzi watia nia wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu 2020.
Killghai amesema, chama hicho kitashirikiana na chama chochote chenye dhamira ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani. “…chama chetu kipo tayari kushirikiana na chama chochote chenye dhamira ya kweli ya kuiondoa CCM na kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi, isiwe kinaingia madarakani kinafanya yaleyale yaliyokuwa yakifanya na CCM,” amesema
Amesema, mchakato wa kugawana majimbo ama kata utafanyika kwa utaratibu watakaokubaliana baina yao na chama ambacho kitaafikiana nacho. Akiizungumzia ratiba ya kura za maoni na uteuzi ndani ya chama hicho, amesema uandaaji wa fomu za utiaji nia umeanza tangu tarehe 5 Mei 2020 na kwamba urejeshaji wa fomu utahitimishwa tarehe 27 Julai 2020.
Amesema chama hicho kimejidhatiti kusimamisha wagombea wa nafasi zote nchi nzima na kuwataka wanachama wote wenye sifa kujitokeza kugombea. “Tunatarajia kuweka wagombea nchi nzima katika ngazi za udiwani, uwakilishi na ubunge.” “Aidha, tunatarajia kusimamisha wagombea Urais wawili, mmoja akisimama kwa ajili ya Urais wa Zanzibar na mwingine akisimama kwa ajili ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Killghai ametumia fursa hiyo, kuwataka wanachama wa chama hicho wenye sifa, kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za kukiwakilisha chama katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.
“Tunapenda kuwahakikishia chama hakina wagombea “wateule.” Kila mwanachama mwenye sifa, atapewa nafasi sawa na mwingine na matakwa ya wajumbe watakaoshiriki kupiga kura za maoni ndiyo ambayo yatapewa kipaumbele labda itokee kwamba kuna sababu za msingi za kutengua maambuzi hayo,”
amesema Kauli ya CUF kuhusu kushirikiana, wameitoa ikiwa zimepita takribani siku nne tangu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufungua milango ya majadiliano na vyama vingine vya siasa ambavyo vinadhamira ya kweli ya kushirikiana kuiondoa CCM madarakani. Jumatano iliyopita ya tarehe 3 Juni 2020, Katibu Mkuu wa Chadena, John Mnyika akizungumza na wanadishi wa habari alisema,
“Tunafungua mlango wa majadiliano na vyama ambavyo vinadhamira ya kweli ya kushirikiana kuiondoa CCM madarakani.” Katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015, CUF na Chadema vilikuwa miongoni mwa vyama vine vilivyoshirikiana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).