Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 7:33 pm

NEWS: CCM ZANZIBAR YATEUWA MAJINA 5 YA URAIS, JECHA APIGWA CHINI

Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoketi jana kimetoka na mapendekezo ya majina ya wanachama watano kati ya 32 waliochukua fomu kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho visiwani Zanzibar, huku jina la aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha likikatwa.

Kwa mujibu wa chanzo cha taarifa kimesema kuwa waliopendekezwa na kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa Omar, Dk. Khalid Salum Mohammed ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo kwa tuhuma za kuanza mbio za urais mapema.

Wengine ni aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa.

majina hayo yatapelekwa mjini Dododma ambapo Julai 9 Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa itapendekeza majina matatu.

Julai 10, Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM itachagua jina moja la mgombea.

Julai 11 – 12, Mkutano Mkuu wa CCM utathibitisha jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa urais Tanzania na upande wa Zanzibar.

Wakati vikao vya juu vya kuchuja majina ya wagombea nafasi ya urais CCM vikianza kesho jijini Dodoma, Kwa upande wa Zanzibar tayari vikao vya juu vya kujadili wagombea urais vilikwishaanza tangu Julai 1- 2 kwa Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar kuketi kuchuja majina.

Julai 3 kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Zanzibar kiliketi kwa ajili hiyo hiyo.