- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
News: CCM yaendelea kuumiza kichwa kushuka kwa kura kwenye uchaguzu mkuu 2015
Dar es Salaam : Chama cha mapinduzi CCM kimeendelea na vikao vya ndani ya chama, KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) imekutana na kujadili tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ikiwamo namna kilivyopoteza majimbo na kata za udiwani.
Kikao hicho ambacho kilipangwa kifanyike kwa siku mbili badala yake kimefanyika kwa siku moja Ikulu Dar es Salaam, huku kiama cha wasaliti ndani ya chama hicho kikiwadia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kikao hicho kilifanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Magufuli.
Nnauye alisema pamoja na mambo mengine kilipokea taarifa hiyo ya tathmini ya uchaguzi ambayo itawasilishwa kesho mbele ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa uamuzi wa mwisho.
Alisema kufanyika kwa tathmini hiyo ya Uchaguzi Mkuu kulitokana na agizo la chama na ngazi za wilaya na mikoa zilikwifanya kufanya tathmini hiyo ya uchaguzi.
“CCM iliagiza viongozi wake wa ngazi zote kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu uliopita.
“Ripoti hizi zimepita hatua mbalimbali na hatimaye Kamati Kuu ya CCM wamekabidhiwa na kuijadili kisha wataikabidhi mapendekezo yao katika kikao cha Hamashauri Kuu ya CCM Taifa kwa uamuzi zaidi,” alisema Nnauye.
Alisema NEC ndiyo itakayotoa mapendekezo na uamuzi wa tathmini hiyo na maelekezo mengineyo.
Kufanyika kwa tathmini hiyo kunatokana na baadhi ya wana CCM ‘kushikana uchawi’ katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Baadhi yao walidaiwa kujihusisha na vuguvugu la kuunga mkono wagombea wa upinzani kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kwa mujibu wa matokeo ya NEC, Rais Dk. John Magufuli alishinda uchaguzi huo kwa kupata kura milioni 8,882,935 (asilimia 58.46) huku aliyekuwa mpinzani wake, Edward Lowassa, akipata kura 6,072,848 (asilimia 39.97).
Chama hicho kikongwe nchini pia kilijikuta kikipoteza baadhi ya majimbo huku vyama vya upinzani vikijikuta vikiongeza idadi ya wabunge tofauti ya mwaka 2010.
Katika uchaguzi huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiliongoza idadi ya majimbo yake na kufikia 34 kutoka 23 ya awali, CUF 25 huku NCC-Mageuzi na ACT-Wazalendo wakipata kiti moja kimoja cha majimbo.
Kwa jumla kambi hiyo ilipata majimbo na wabunge wa viti maalumu wapatao 116.
CCM ilijikuta ikibaki na majimbo 188 huku idadi ikipunguzwa hadi kwenye mgawanyo wa viti maalumu na kubaki na viti maalumu 64.
Nape pia aliviasa vyombo vya habari kwa kuvitaka kuacha taarifa za kuokoteza zinazopikwa na watu wenye nia ovu.
Katika kikao hicho cha NEC, inatarajiwa Rais Dk. John Magufuli, huenda akafanya mabadiliko ya sekreterieti ya chama baada ya kufanya uteuzi kwa baadhi ya wajumbe wake ambao amewapa nafasi ndani ya Serikali.
Kutoka Mtanzania