Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:19 pm

NEWS: BODI YA MIKOPO YATANGAZA ORODHA YA WANAFUNZI WALIOPATA MIKOPO

Dar es salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza leo (Jumapili, Oktoba 17, 2021) orodha ya Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi 37,731 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 99.9 bilioni kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaotarajiwa kuanzia wiki ijayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kuwa kati ya wanafunzi hao (37,731), wanaume ni 23,379 sawa na asilimia 62 na wanawake ni 14,352 sawa na asilimia 38.

Badru ameongeza kuwa HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili. Unaweza kuangalia kupitia Acc hii https://olas.heslb.go.tz


“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” amesema Badru.

Tarehe ya kutolewa orodha ya Awamu ya Pili

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Pili, Badru amesema imepangwa kutolewa Alhamisi, Oktoba 21, 2021 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao ya SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Orodha hii ya kwanza inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wana udahili wa chuo kimoja … tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya pili katika siku mbili zijazo, yaani Jumatamo, Oktoba 20, 2021,” amesema Badru.

TZS 570 Bilioni zimetengwa kwa mikopo ya elimu ya juu 2021/2022

Kwa mujibu wa Badru, Serikali imetenga TZS 570 bilioni kwa ajili ya mikopo ya jumla ya wanafunzi 160,000. Kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wapya na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.

Fedha zimeanza kutumwa vyuoni

Wakati huohuo, Badru amesema HESLB imeshapokea fedha kwa ajili ya malipo ya wanafunzi na taratibu za malipo zimeanza ili fedha hizo ziwe zimefika vyuoni kuanzia Jumanne, Oktoba 19, 2021.