Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 4:00 pm

NEWS: BOBI WINE AACHILIWA HURU KWA DHAMANA, ASHTAKIWA KWA KUENEZA CORONA

Mwanasiasa wa Upinzani nchini Uganda ambaye pia ni Mgonbea Urais wa nchi hiyo Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ameachiliwa huru kwa dhamana mara baada ya Mahakama moja mashariki mwa Uganda kumshtaki kwa kosa la kusambaza ugonjwa wa Corona(Covid19).

Bobi Wine alikamatwa katika mkutano wa kampeni Jumatano akishtumiwa kwa kukiuka miongozo ya kudhibiti ugonjwa wa virusi vya corona kwenye mkusanyiko wa hadhara.

Hadi kufikia sasa watu 28 wamethibitishwa kufariki dunia kote nchini humo wakati wa maandamano yaliyokuwa yakidai kuachiliwa huru kwa Bobi Wine huku wengine zaidi ya 500 wakikamatwa, kulingana na jeshi la polisi.

Maandamano hayo ya kudai kuachiliwa huru kwa Bobi Wine, yalisambaratishwa kwa kutumia vitoza machozi na wakati mwingine risasi zilitumiwa.

Awali, naibu msemaji wa jeshi, Kanali Deo Akiiki aliviambia vyombo vya habari kuwa wanajeshi watapelekwa katika barabara zote kuu zinazoingia mjini.

Januari 2021, Uganda itakuwa na uchaguzi mkuu wa urais lakini wiki za kwanza za kampeni tayari zimekubwa na vurugu na ghasia.