Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 2:50 pm

IGP SIRRO: NIKO TAYARI KUTOA ULINZI KWA LISSU NA LEMA, WARUDI TUJENGE NCHI

Jeshi la Polisi nchini limesema hali ya Utulivu na Amani imeendelea kutawala tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 na kuwashukuru Watanzania kwa kutoshawishika kujiingiza katika vurugu na maandamano yaliyotangazwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa yaliyokuwa na lengo la kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro akizungumza na Waandishi wa habari wakati akitoa tathmini ya hali ya nchi baada ya kumalizika kwa Uchaguzi mkuu wa oktoba 27 na 28 Tanzania bara na visiwani amesema hali ni Shwari lakini hata hivyo Jeshi la Polisi linawashikilia watu 254 nchini kote baada ya kujihusisha na vurugu baada ya uchaguzi.

Aidha IGP Sirro amezungumzia madai yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutishiwa maisha sio ya kweli na jeshi hilo limesema liko tayari kutoa ulinzi kwa viongozi hao pamoja na kuyafanyia kazi madai hayo ili wahusika wakamatwe.

Kama utakumbuka viongozi wakuu wawili wa Chamdema Godbless Lema ambaye alikuwa mbunge wa Arusha mjini na Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya chadema Tundu Lissu walitangaza kutishiwa amani na kuamua kukimbilia uhamishoni ili kunusuru maisha yao.

Akizungumzia hali ya Usalama Mkoani Mtwara katika vijiji vinavyopakana na Msumbiji ambako kumekuwepo na matukio ya uhalifu na Mauaji amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaendesha Operesheni maalum huku akiwaonya vijana wa Kitanzania wenye nia ya kujiunga na kundi hilo.