Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 12:59 pm

AFYA: VYAKULA VYA KUONDOA GESI MWILINI

Kuna baadhi ya vyakula vya kuondoa hili tatizo kama linakusumbua kwa muda mrefu.

Kulingana na namna tunavyoishi na ulaji wa vyakula husababisha tumbo kuchafuka kwa kujaa gesi, kuuma na hata kunguruma, unahisi unahitaji kunywa dawa ili kutuliza tatizo hilo lakini unaweza kutumia vyakula badala ya dawa za kisasa ambazo hutuliza dalili na huliondoa tatizo kabisa.

CHANZO CHA TATIZO

Kabla ya kukimbilia kwenye tiba, ni vizuri kwanza kujua chanzo cha tatizo na ni muhimu kujua ni vyakula gani ukila vinasababisha matatizo ya tumbo. Aina ya vyakula inaweza kutofautiana kati ya watu mbalimbali lakini kuna aina ya vyakula vinavyojulikana zaidi kusababisha matatizo ya tumbo.

Vyakula na vinywaji vinavyochangia tumbo kujaa na ukosefu wa choo kwa muda mrefu huwa ni soda, tembo hasa bia, vyakula vyenye mafuta mengi na vyenye chumvi nyingi.

Vyakula hivyo vinapoingia tumboni, huwa na tabia ya kuchelewesha usagaji wa chakula na uondoaji wa uchafu kwenye utumbo, hivyo huwa kikwazo katika mfumo mzima wa usagaji chakula kwa urahisi.

Ili kujiepusha na matizo ya tumbo ya muda mrefu na hata kuzuia uwezekano wa kuumwa na tumbo mara kwa mara, unashauriwa kula vifuatavyo, karibu kila siku ili kulifanya tumbo lako kuwa safi wakati wote:

Papai

Baadhi ya utafiti uliyopo, unaonesha kwamba ‘enzyme’ kwenye papai husaidia usagaji wa chakula tumboni. Tunda hili, lenye ladha tamu na harufu nzuri, huboresha mfumo wa usagaji chakula, husafisha utumbo, huzuia magonjwa ya uvimbe tumboni na huimarisha mfumo wa kinga ya mwili.

Vitamini na virutubisho vya papai vina faida nyingi, lakini faida kubwa ya papai ipo kwenye kirutubisho aina ya ‘Papain’ ambacho hujulikana kwa uwezo mkubwa Ilionao wa usagaji wa chakula tumboni.

Mtindi (yogurt)

Hata kama wewe si mpenzi wa mtindi, jaribu kunywa na utaupenda. Huwa na uwezo wa kuondoa matatizo ya kujaa gesi tumboni pamoja na matatizo mengine. Mtindi mzuri ni ule ambao haujachanganywa na ladha au vitu vingine kwa lengo la kuongeza ladha. Bakteria asilia waliomo kwenye maziwa ya mtindi ndiyo hufanya usagaji wa chakula kuwa mwepesi.

Mwisho, ili kupata faida ya papai na mtindi kama ilivyoelezwa hapo juu, ni vizuri ukala mara kwa mara kama sio kila siku, kabla au mara baada ya kula vyakula ambavyo vinaweza kukuletea shida tumboni, au ukaweka mazoea ya kula kila siku ili kuliweka tumbo lako katika hali salama