Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 8:18 pm

NEWS: SPIKA NDUGAI AWATAKA WAPINGAJI WA TOZO KULETA NJIA MPYA YA KUPATA FEDHA

Dodoma. SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amewataka watu wanaopinga ongezeko la tozo mpya ya miamala ya simu, waeleze njia mbadala itakayowawezesha Serikali kupata fedha za kuwaletea maendeleo wananchi.

Ndugai, ametoa kauli hiyo hii leo Ijumaa tarehe 23 Julai 2021, wakati akizungumza katika kikao kazi cha Mkoa wa Dodoma, kilichoandaliwa na mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka.

Spika Ndugai amesema, Bunge lilipitisha sheria ya tozo hiyo, ili Serikali ipate fedha za kuibadilisha Tanzania kimaendeleo.

“…wewe unayepinga tozo hii, tupe njia mbadala tutapata wapi fedha. Maamuzi haya tumeyapitisha kwa nia njema kabisa, tuwe na Taifa ambalo ni tofauti,” amesema Spika Ndugai.

Tozo hizo zinazotozwa katika miamala ya simu, zilianza kutumika kuanzia tarehe 15 Julai 2021.

Ambapo Serikali inatoza kuanzia Sh. 10 hadi 10,000, katika muamala wa kutuma au kutoa pesa, kulingana na thamani ya muamala wa fedha husika.

Kupitia tozo hiyo, Serikali inatarajia kukusanya zaidi ya Sh. 600 bilioni, katika mwaka wa fedha wa 2021/22, ambazo zitatumika katika kuimarisha huduma za afya, miundombinu ya barabara na elimu.