Home | Terms & Conditions | Help

Wed Apr 09 2025 2:57:46 PM

NEWS: LISSU KUREJEA TANZANIA

Dar es salaam. NAIBU kiongozi wa chama kikuu cha upinzani hapa nchini, Chadema, Tundu Lissu amewaahidi wanachama wa chama hicho kuwa anampango wa kurejea nyumbani Tanzania ‘hivi karibuni’.

Kauli hii ya Lissu inakuja ni kufuatia kile kinachoonekana kuwa makubaliano kati yake na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kukutana Februari 17,2022 nchini Ubelgiji.

Bw Lissu, ambaye alinusurika kifo mjini Dodoma mnamo 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, amekuwa akiishi uhamishoni nchini Ubelgiji.

Akiongea kwenye mahojiano na chombo cha STAR TV Cha jijini Mwanza, Bw Lissu alisema atarejea nyumbani “hivi karibuni” kwa sababu ana imani kwamba Rais Suluhu atamhakikishia usalama wake.

Mwanasiasa huyo ambaye ameishi Ubelgiji tangu 2017, alimmiminia sifa rais huyu kwa kuelekeza taifa katika mkondo mzuri kiuongozi.

“Wakati huu hatuhesabu miaka kabla ya kurejea kwangu nyumbani. Hatuhesabu miezi. Hatuhesabu wiki,” Bw Lissu akasema, kuashiria kuwa huenda akarejea Tanzania siku chache zijazo.

Kiongozi huyo wa Chadema alisema hayo karibu mwezi mmoja baada ya kukutana ana kwa ana na Rais Suluhu jijini Brussels, Ubelgiji.

Wakati wa mkutano huo uliofanyika Februari 16, 2022, Bw Lissu alimwomba rais huyo kumhakikishia kuhusu usalama wake.

Hii, kulingana na mwanasiasa huyo, ni kwa sababu wale waliojaribu kumuua bado hawajulikani na hamna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

“Rais Samia, aliahidi kushughulikia suala hili linalonihusu (usalama wangu) na nina matumaini kuwa atafanya hivyo,” Bw Lissu akasema.“Japo ana kazi nyingi za kufanya, sidhani atapuuza ombi langu,” akaongeza.

Bw Lissu alimtaja Rais Suluhu kama kiongozi anayesikiza ushauri kwa makini huku akielezea matumaini yake kwamba ataheshimu misingi ya demokrasia na haki.Mapema mwezi huu – Machi 2022 – serikali ya Tanzania ilimwachilia huru mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu walioshtakiwa pamoja.

Kiongozi huyo alikuwa amezuiliwa rumande kwa miezi minane kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kigaidi na uhalifu wa kiuchumi.

Hata hivyo, wakosoaji wa serikali walidai mashtaka hayo yalikuwa ya kuwekelewa na hayakuwa na msingi wowote.Kuachiliwa huru kwa Bw Mbowe kulitanguliwa na mazungumzo yaliyoshirikisha viongozi wa kidini, Bw Lissu na Rais Suluhu.

Viongozi hao wa kidini walimtaka rais huyu kutumia mamlaka yake kutupilia mbali kesi dhidi ya Bw Mbowe na washirika wake watatu.

Katika mkutano kati yake na Rais Suluhu, Bw Lissu alimtaka “kuwarejesha nyumbani” viongozi wengine wa upinzani waliotoroka Tanzania kusaka hifadhi katika mataifa ya nje.

Naibu huyo wa kiongozi wa Chadema, pia alimshukuru Rais Suluhu kwa kumsaidia kupata paspoti mpya baada ya kupoteza paspoti yake ya zamani akiwa nchini Ujerumani.

“Kuna matumaini makubwa kwamba siasa nchini Tanzania zitaboreshwa chini ya uongozi wa Rais Samia,” akasema Bw Lissu.

Lakini alisema ili Rais aendeleze mtindo huo wa utendakazi, anahitaji uungwaji mkono kutoka kwa vyama vya upinzani.

“Alianza vizuri, lakini angali na kazi nyingi za kufanya ili kurejesha sifa ya Tanzania kama taifa linaloheshimu demokrasia. La muhimu ni kwamba anahitaji uungwaji mkono kutoka kwetu,” akasema Bw Lissu.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo alisema kuwa katiba mpya ndio itakuwa suluhu kwa changamoto zinazohusiana na ukosefu wa uongozi bora.