Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:46 pm

UTAFITI: NJIA 5 ZA KUMFANYA MTOTO APENDE KULA.

Kuwa mzazi ni jambo jema, ila kulea mtoto si kitu rahisi, haswa akiwa ndio mtoto wa kwanza. Wengi wetu tunalea watoto kutokana na maelekezo ya watu wenye uzoefu na malezi kwa muda mrefu. Tatizo linakuja pale ambapo mbinu wanazotumia zinapoleta madhara makubwa kuliko faida. Mie nasisitiza kuwa, kulea si rahisi, maana kila mtoto ana tabia zake na ni vizuri mzazi akiwa na muda wa kujua nini hasa atakacho mtoto kabla ya kufuata ushauri usio wa kitaalamu na kusababisha madhara makubwa.

Je ulishawahi kushauriwa kumkaba mtoto wakati anapogoma kula ? Kama ulishaambiwa basi fahamu si ushauri mgeni, mie pia huwa naupata kila siku. Ila linapokuja swala la mtoto, huwa napenda kupata ushauri wa wataalamu, maana watoto hawafanani. Si kila mbinu inaweza kufanya kazi kwa kila mtoto, hivyo ni bora kuchanganya akili yako katika kila ushauri unaopewa kabla ya kuufanyia kazi.

Katika mada yetu ya leo napenda tuzungumzie mbinu chache za kumfanya mtoto apende kula bila kukabwa. Wote tunafahamu kuwa chakula ni kitu muhimu sana kwa makuzi bora ya mtoto ili awe na siha njema, hivyo kila mzazi anafurahi pale mwanae anapokula vizuri bila matatizo. Wazazi wengi hujisikia vibaya sana pale mtoto anaporinga au kukataa kabisa kula chakula, sababu kutokula chakula vizuri humfanya mtoto kuwa mdhoofu na rahisi kupata magonjwa.

Kwanini watoto wanakataa chakula ?

Ili kuweza kutatua tatizo ni vizuri kutafuta kitu kinachosababisha tatizo, je kwanini watoto wengine wanakataa kula ?

Mie sikuwa na jibu la haraka, bali nikaona ni vizuri kwenda kumuona daktari bingwa wa masuala ya watoto ambaye ameshakutana na matatizo mengi kama haya. Daktari alisema kuwa kuna sababu nyingi ambazo zinaweza kumfanya mtoto akatae kula, hizi hapa ni chache tu:

  • Mtoto anakuwa ameshiba na hajisikii hamu ya kula. Hii inawezekana kusababishwa na mtoto kula vitu vidogo vidogo mara nyingi hivyo kuzuia njaa na kumzuia kula chakula vizuri.
  • Hapendi chakula anachopewa sababu hajakizoea au hakifurahii. Watoto wengi wanaweza kukataa kula mboga za majani, lakini ni muhimu sana ale sababu ni chakula pekee kinachomfanya akue vizuri.
  • Anaumwa na amepoeza hamu ya kula. Ugonjwa ni moja ya sababu kubwa za kumfanya mtoto kugoma kula.
  • Amechoka chakula anachopewa hivyo kutokifurahia tena. Kula chakula cha aina moja muda mrefu inaweza kuwa ni sababu kubwa ya mtoto kugoma kula. Hata kama anafurahia chakula, wakati mwengine anaweza asipende tena kula. Hivyo ni vizuri kuweka vyakula tofauti ili mtoto apate ladha na virutubisho tofauti.
Ni muhimu kuzingatia kuwa, katika mazingira yeyote yale usimlazimishe mtoto kula na ni hatari kubwa kumkaba ili ameze chakula. Kulazimisha mtoto kula ni kumjengea tabia ya kuchukia chakula. Mtoto akishajenga tabia hii hawezi kuacha sababu atakuwa anahusisha chakula na adhabu. Sababu hakuna mtu anayependa adhabu, atakuwa anachukia chakula cha aina yeyote. Matokeo yake ni kuwa mtoto atajenga tambia mbaya zaidi ya kukataa kula chakula cha aina zote. Pia, kumkaba mtoto kunaweza kuleta matatizo makubwa kama vile kufanya chakula kuingia kwenye njia ya hewa, hii itakuletea kesi zisizo za lazima.

Jinsi ya kutatua tatizo

Kutatua tatizo huanzia kwenye kujua tatizo liko wapi. Ushauri nasaha aliotoa daktari ni kuwa, hakuna muarobaini wa kutibu hii tabia, bali ni swala la kujaribu mbinu mbalimbali ili kuweza kujua kitu kimoja kinachoweza kuwa suluhisho la ukataaji wa kula wa mtoto.

Katika njia muhimu alizopendekeza ni pamoja na hizi hapa:

1. Kubadilisha vyombo vya chakula vya mtoto

Daktari alisisitiza kuwa, mtoto huvutiwa zaidi na rangi, hasa kwenye vitu anavyotaka kula. Mtoto anaweza kuchoka kula chakula sababu anatumia chombo kimoja kila siku, hii haijalishi kama chakula kinabadilika au la. Ni muhimu kumuandalia mtoto chakula kwenye vyombo vyenye rangi na maumbo tofauti. Na ushauri wa daktari ni kuwa, usirudie chombo kwa wiki nzima, kama inawezekana. Hii inamfanya mtoto kuona utofauti wakati wa kula, na kumfanya apate hamu ya kula.

Mfano, unaweza kutumia bakuli, vikombe, sahani, vijiko vyenye rangi tofauti ili kumfanya aone anakula katika mazingira tofauti na hii humfanya awe na hamu kula chakula zaidi.

2. Watoto wale pamoja na familia

Watoto hupenda kuiga wazazi. Mara nyingi sana watoto hupewa vyakula wale wakiwa wenyewe wakati watu wengine wanaendelea na shughuli za kawaida. Hii inaweza kumfanya mtoto kupendelea zaidi kucheza kuliko kula. Ni muhimu kumlisha mtoto wakati familia nzima imekaa mezani au jamvini tayari kwa kula. Katika muda huu mtoto atakula vizuri bila vikwazo, maana kila mmoja anakula.

Vilevile, watoto wengine (umri wa miezi 10 hadi miaka 2) hupendelea kula vyakula wanavyokula watu wazima, hata kama haviwafai, na kugoma vyakula vya watoto. Ni bora kumuandalia chakula kinachofanana na unachokula wewe na kumpa ili apate kufurahia. Huwezi kubishana na mtoto, ingawa huwezi kumpa kila kitu anachotaka pia. Ila jaribu kutumia mbinu tofauti ili apate kula na kuridhika. Afya yake ni bora kuliko kitu kingine kwenye maisha yake kwa muda huu.

3. Jaribu kumsoma mtoto anapenda nini

Kila mzazi ana jukumu la kumsoma mwanae anapendelea nini. Ili kuweza kumfanya mtoto ale vizuri, ni vyema kubadilisha vyakula kila wakati – siyo kila siku. Mara nyingi watoto huchukua muda kuzoea chakula, hivyo ni vizuri kumpa mtoto chakula kwa muda wa siku 2 hadi 3 na kumbadilishia na chakula kingine. Hii inasaidia mtoto kuonja ladha ya chakula. Anaweza kukipenda au kukichukia. Kama atakataa ladha ya chakula kipya, usikate tamaa, jaribu kumpa tena baada ya siku moja au mbili, unaweza kukuta akaipenda ladha na akala chakula bila tatizo.

Usikate tamaa kwenye kumpa mwanao upendo wako kama mzazi. Jaribu kila njia unayoweza na usife moyo. Watoto ni wagumu kuwaelewa na inachukua muda, lakini pale unapofikia hatua ya kujua anachopenda utakuwa umepata jibu zuri jinsi ya kuendelea kumlea mwanao.

4. Epuka kumpa vitu vitamu kati ya milo

Watoto wengi wanapenda kula vitu vidogo vidogo (pipi, biskuti, juisi, keki n.k.) kila mara. Hivi vitafunwa vinaweza kumfanya mtoto azibe njaa na kutokuwa na hamu ya kula chakula muda unapowadia. Ili kuzuia hii tabia, ni bora kuacha kumpa mtoto vitu vidogo vidogo kati ya milo ili kumfanya kuwa na hamu ya chakula muda unapowadia.

Mara nyingi inashauriwa kumlisha mtoto mara 4 hadi 5 kwa siku. Hii ni vizuri sababu mwili wa mtoto unakuwa unahitaji virutubisho vingi mara kwa mara kwa kusaidia kukua. Ni vizuri kumpa mtoto chakula bora kuliko kumjaza tumbo na vyakula vyenye sukazi zisizo na kazi mwilini.

5. Msikilize mtoto anachotaka

Mara nyingi mzazi au mlezi unaweza kudhani kuwa unajua zaidi kiwango cha chakula anachotakiwa kula mtoto kuliko hata mtoto mwenyewe. Hili linaweza kuwa tatizo kubwa litakalopelekea mzazi kumlazimisha mtoto kula chakula kingi kupita kiasi. Fahamu kuwa, watoto wanajua kiwango cha chakula kinachowatosha na wakati gani ni muafaka wa kula. Hivyo, itakuwa rahisi kwako kama ukimsikiliza mtoto anataka nini, kuliko kulazimisha kile unachotaka wewe. Hakuna mtoto anayeweza kuvumilia kukaa na njaa. Watoto wote huhitaji chakula ili kucheza na kufurahi na wenzao. Hivyo basi, pale anakuwa na njaa atasema, au kulia, na ndio muda muafaka wa kumpa chakula unachotaka.

Swala muhimu la kuzingatia ni kuwa, katika mazingira yeyote, usimlazimishe mtoto kula. Usimkabe. Kulazimisha mtoto kula ni kumjengea tabia ya kuchukia chakula. Na akishajenga tabia hii hawezi kuacha sababu atakuwa anahusisha chakula na adhabu. Hakuna mtu anayependa adhabu. Hivyo, watu wengi wanaopenda kulazimisha mtoto kula kwa kumkaba huwa wanajenga tatizo kubwa zaidi ya lile la kula tu.