Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:35 pm

NEWS: WANANCHI WA HANANG WAIPONGEZA SERIKALI UJENZI WA BARABARA ZA LAMI

HAVING: Diwani wa Kata ya Gagana wilayani Hanang Mhe. Isaya Mbise ameishukuru Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kata ya Ganana wilayani humo kwa miradi wa ujenzi na matengenezo ya barabara ikiwemo barabara ya lami yenye urefu wa Km. 3.02 ambazo zimewasidia katika usafiri na usafirishaji.


Mhe. Mbise amesema kwamba ujenzi wa barabara umeweza kuwasaidia wananchi wa Kata hiyo pamoja na wilaya kwa ujumla kwani wananchi wengi ni wakulima na kabla ya lami walikuwa na barabara za vumbi ambapo zinahitaji kufanyiwa maboresho kila wakati.

"Kufanya ukarabati wa barabara kila wakati ni gharama kwa Serikali na tunajua kufanya matengenezo ya barabara nchi nzima ni changamoto, sasa kwa ujenzi wa lami itatusaidia kwa kipindi kirefu, lakini tuipongeze Serikali kwa kazi kubwa waliotufanyia.

Hata hivyo Diwani huyo hakusita kuishukuru Serikali kwa kazi waliyoifanya ya kurejesha miundombinu katika kata yake pamoja na kata nyingine ambapo ziliathirikiwa wakati wa maporomoko ya mlima Hanang.

"Kwakweli tunaishukuru sana Serikali na Rais wetu Dkt. Samia kwa kazi iliyofanyika katika kata zote zilizoathiriwa, wamejitahidi kuirejesha miundombinu na hata sasa hivi wananchi wanaendelea na shughuli zao za maendeleo kama kawaida".

Aidha, amesema wilaya kuwa na barabara nzuri kama hizo imemrahisisha mwananchi kupeleka mazao kwenye masoko na hivyo kuwainua kiuchumi.

Aliongeza kusema kuwa katika miradi hiyo TARURA iliwashirikisha katika kila hatua na hata hivyo wananchi kupata ajira kupitia miradi hiyo.

"Pia kabla ya kuanza kwa miradi hii wananchi tulijengewa uelewa na kufahamu miradi hii ni ya kwetu na hivyo tuna ahadi kuitunza ili idumu kwa muda mrefu".Aliongeza Mhe. Mbise.

Naye, mwendesha bodaboda wa mji wa Kateshi Bw. Festo Manda amesema wanaishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hizo kwani awali tope lilikuwa linawasumbuwa katika uendeshaji wa vyombo vya moto.

"Wilaya ya Hanang haijawahi kuwa na barabara ya lami tangu kuanzishwa kwake zaidi ya barabara kubwa ya Babati-Singida, tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuturahisishia maisha wananchi tunaishukuru kwa maendeleo haya na tuna imani mji wetu wa Kateshi utakuwa na barabara nyingi za lami.

Pia Bi. Yasinta Bayo mkazi wa Kata ya Ganana amesema sasa hivi wana barabara za lami ambazo zinaenda kwenye mitaa mbalimbali tofauti na zamani ambapo mtu akibebwa na bodaboda ilikuwa ni ugomvi na hata walikuwa wakikataa kuwafuata ila sasa hivi hata usiku unafuatwa na imewarahishia kwenda vituo vya afya na hospitali ya wilaya.

Awali, Meneja wa TARURA Wilaya ya Hanang Mhandisi Paul Mlia amesema katika Wilaya yake hivi sasa wameweza kujenga barabara za lami na kufikia Km. 3.02 pamoja na kuweka taa za barabarani 47 ambapo awali mji huo haukuwa na barabara za lami kabisa.

Mhandisi Mlia ameendelea kusema kuwa TARURA wilayani hapo wanahudumia mtandao wa barabara Km. 1050.5 na kati ya hizo barabara za changarawe Km. 349.69 na udongo Km. 697.79 na katika kipindi cha miaka mitatu wamefanikiwa kuongezewa bajeti ya ujenzi na matengenezo ya barabara na kuwezesha Km. 96 za barabara kufunguliwa.