Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 1:47 am

UTAFITI: FAIDA NA MBINU ZA KUWEZA KUAMKA MAPEMA.

Waswahili tunao msemo usemao, Siku njema huonekana asubuhi. Ni msemo wa kale ambao tafsiri yake halisi inaweza kutofautiana baina ya mtumiaji mmoja kwenda mwingine. Huo ndio utamu wa lugha na misemo ya kwetu. Tunaweza kutofautiana lakini wote tukawa sahihi, angalau kwa mapana yake.


Pamoja na tofauti kadhaa zinazoweza kujitokeza katika tafsiri, nina uhakika kwamba wengi tutaelemea katika tafsiri rahisi ambayo ni kwamba unavyoianza siku ndivyo utakavyoimaliza. Hisia na vitendo vyako unapoianza siku yako vina mengi ya kusema kuhusu itakavyokwenda na itavyofikia ukingoni.

Ukiamka na kujihisi mchovu,ukaichukia siku hata kabla haijaanza,ni wazi kwamba utakuwa umejiweka mwenyewe kwenye mtego wa kuwa na siku mbaya! Hutofanikisha malengo yako.Kazini unapokwenda mambo yanaweza kwenda mrama.Kwanini? Umeiandaa vibaya siku yako.Ikitokea mwenzako fulani iwe kazini au shuleni akakuambia mbona leo unaonekana kama unaumwa au umechoka(hata kama anakutania tu) ndio kabisaaa anakuwa amekumaliza.

Kwa upande mwingine, siku njema huonekana asubuhi unaweza kuwa msemo unaoonyesha nguvu ya utabiri tuliyonayo sisi kama wanadamu.Tunazo hisia.Unaweza kuhisi kwamba kitu fulani unachokifanya au unachoacha kukifanya kinaweza kuwa na matokeo yasiyopendeza. Kila mmoja wetu anazo nguvu za utabiri.Tofauti ni jinsi tunavyozitumia,kuziamini au kuzifanyia kazi.

Bahati nzuri ni kwamba binadamu tumepewa uwezo mkubwa wa kunyumbulisha dunia na mambo mbalimbali.Sasa ufanyeje ili uianze siku vizuri? Wataalamu mbalimbali wa mambo ya saikolojia na utabibu wanakubaliana kwamba ukiianza siku yako mapema, itakuwa nzuri! Kuanza siku mapema, kwa mapana na marefu kunajumuisha kuamka mapema na kuwaza vyema.

Leo nimeamua kuongelea umuhimu wa kuamka mapema kwani kama nilivyotangulia kusema hapo juu,wataalamu wengi wanakubaliana kwamba kuamka mapema ni msingi wa kuwa na siku nzuri,maisha mazuri na kubwa zaidi,afya nzuri.Watu wengi ambao tunawaita “waliofanikiwa maishani” na hata matajiri wakubwa hapa duniani,wanalo jambo moja linalofanana. Katika kuwafuatilia(kupitia makala za magazetini,vitabuni na hata mahojiano yao katika televisheni) wote wanakiri jambo moja.Wote ni wa kwanza kudamka(early birds). Kwanini?Bila shaka kuna sababu.

Pengine baada ya kusoma kichwa cha habari umeshajiuliza; kwanini niamke mapema? Sababu ya Kwanza ni kwamba unapoamka mapema, unapata muda mzuri wa kujiweka sawa,kuipanga siku yako vyema. Imeshawahi kukutokea ukakurupuka usingizini na kukuta muda umeshakwenda na umechelewa kwenda unapotakiwa kwenda iwe ni kazini,shuleni au kwingineko? Umeshaona jinsi mpangilio wako wa mambo unavyokwenda kombo? Unapofika ofisini kwa mfano, unakuwa hata kuamka vizuri hujaamka bado na kila mtu anakutolea macho kwa sababu hata nywele hukukumbuka kuchana? Ungeamka mapema,ukaipanga siku yako vyema yote hayo yasingekukuta.

Faida ya pili ni kuweza kutumia ukimya wa asubuhi. Umeshawahi kudamka asubuhi ukaona jinsi palivyo na utulivu wa aina yake? Amini usiamini,ukiutumia ukimya huo wa asubuhi kuwaza na kupanga mambo yako,ni wazi kwamba utafanikiwa zaidi. Akili ya binadamu imetengenezwa ifanye vizuri zaidi panapokuwa na utulivu. Wenzetu wa magharibi ndio maana wakaja na msemo wa Silence is Golden.

Tatu,wataalamu wa afya wanasisitiza sana kuhusu kifungua kinywa(breakfast). Huo ndio mlo muhimu zaidi katika siku. Ni wazi kwamba ukiamka mapema, utapata muda mzuri wa kuandaa na kisha kupata kifungua kinywa kwa utaratibu unaofaa bila papara kitu ambacho ni muhimu kwa afya yako.

Nne, utapata muda wa kufanya mazoezi. Ni dhahiri kwamba mazoezi yanaweza kufanyika katika muda wowote. Hata hivyo,mazoezi ya asubuhi yana mchango mkubwa zaidi katika suala zima la siku nzuri. Ukiamka mapema na kufanya mazoezi(mepesi tu na kwa nusu saa tu) utakuwa umeweka akili na mwili wako tayari kuikabili siku.Kingine cha kuzingatia hapa ni kwamba mazoezi ya jioni au muda mwingine yanaweza kutofanyika kutegemea na jinsi siku ilivyokwenda.Ya asubuhi ni vigumu kutofanyika kwa sababu siku ndio kwanza imeanza.Hakuna kisingizio.

Tano ni kuepukana na foleni. Miji yetu siku hizi ina magari mengi kuliko barabara. Jijini Dar-es-salaam kwa mfano, safari ya dakika 15 inaweza kukuchukua saa nzima kama sio masaa mawili. Ukiamka mapema ni wazi kwamba utaweza kuondoka nyumbani mapema na hivyo kuepukana na foleni za kutisha za asubuhi. Kumbuka kwamba unapokwama kwenye foleni na hali unajua kabisa kwamba unachelewa, presha hupanda, akili huchanganyikiwa,utulivu na amani ya nafsi huondoka.Huo unaweza kuwa mwanzo wa kuwa na siku mbaya.

Sita ni kuweza kuwahi katika miadi yako. Suala la kutunza muda nimeshaliongelea siku za nyuma. Unapowahi katika miadi yako unaheshimika. Unapochelewa katika miadi wapo ambao watakuona hufai. Bahati mbaya hao ni wengi zaidi. Ukiamka na kupanga siku yako mapema,utawahi na kufanikiwa katika miadi yako yote.

Naam.Baada ya kuona faida mbalimbali(orodha inaweza kuongezeka) za kuamka asubuhi, swali linalofuata ni je,nifanyeje ili niweze kuamka mapema? Hili ni tatizo au changamoto kubwa miongoni mwa wengi wetu. Hatutaki kusikia kwamba kumekucha na ni muda wa kuelekea aidha kazini,shuleni au popote pale tunapotakiwa kwenda. Tunatamani tuendelee kulala.

Kama nilivyotangulia kusema hapo juu,wataalamu wengi wa masuala ya saikolojia na hata utabibu wanakubaliana kwamba kuamka mapema kuna faida nyingi za kiafya,kiakili,kiuchumi nk.Hata hivyo bado kuna tofauti mbalimbali miongoni mwa wataalamu hao hao kuhusu jinsi ya kufikia malengo ya kuweza kuamka mapema. Hata ninapoandika makala hii hivi leo,naamini kwamba hata wewe unaweza usikubaliane na mbinu nitakazoshauri hapa;

  • Anza taratibu: Kama kuamka mapema ni mojawapo ya malengo yako ya mwaka huu,basi unashauriwa kwamba usianze ghafla.Yaani kama mpaka hapo jana ulikuwa ukiamka saa mbili asubuhi,basi usije ukaenda nyumbani leo na kujaribu kuamka saa kumi na moja asubuhi. Anza taratibu.Badala ya kuamka saa mbili,jaribu kuanza kuamka saa moja na nusu.Kisha siku inayofuata amka saa moja kamili. Endelea kufanya hivyo mpaka utakapofikia malengo yako.
  • Lala Mapema: Kawaida binadamu anatakiwa au anashauriwa kupata japo masaa nane ya usingizi. Najua kwamba hili huwa ni gumu kwa watu wengi kutokana na aina ya maisha tunayoishi. Pengine ni kutokana na kazi au kutopata usingizi kutokana na kuwa mawazo mengi(stress) au matatizo mengine ya kijamii(haya tutakuja kuyaongelea siku za mbeleni). Sasa ili kupata muda mwingi wa kulala na uweze kuamka mapema ukiwa na nguvu na ari,unashauriwa kulala mapema. Jipangie vizuri muda wako. Mbinu mojawapo ya kufikia lengo la kulala mapema ni kuzima taa. Binadamu wengi huanza kusinzia mara taa zinapozimwa.Kwa hiyo zima taa mapema na hivyo utalala mapema.
  • Weka alarm mbali na unapolala: Kutokana na maendeleo ya tekinolojia, siku hizi wengi wetu hatutegemei kuamshwa na “mlio wa jogoo”. Badala yake wengi tunatumia alarms.Unaitegesha tu na muda ukifika itawaka kwa wimbo au makelele kuashiria kwamba muda wa kuamka umeshawadia. Sasa kama alarm clock yako ipo karibu na ulipolala, nafasi ya wewe kunyanyua mkono,kuizima na kuendelea kulala ni kubwa. Badala yake ukiiweka mbali,itakubidi uamke kwani itakusumbua.Ukishanyanyuka kitandani ni vigumu kurudi hususani kama ulishapangilia ratiba nzima ya siku yako kabla hujaenda kulala hapo jana.
  • Tafuta sababu ya kuamka mapema: Kama huna sababu ya kuamka mapema,inaweza kuwa ngumu hata kudhamiria kuamka mapema. Kwa kuangalia faida za kuamka mapema kama nilivyozitaja hapo juu(na nyingine ambazo sikuzitaja) utagundua kwamba kuamka mapema ni kwa faida yako.Una kazi unatakiwa kufanya?Una kitabu unatakiwa kusoma?Unataka kukwepa foleni ya asubuhi ? Unayo miadi ambayo unatakiwa kuitimiza asubuhi na mapema? Hizo zaweza kuwa sababu za kutosha kabisa kukuamsha mapema. Kumbuka pia…siku njema huonekana asubuhi.
Kabla sijamalizia naomba niongelee tena ushauri wa kulala mapema ili kuamka mapema.Wataalamu mbalimbali wa hivi karibuni wanashauri kitu tofauti kidogo.Wao wanasema kwamba lala pale utakapohisi kwamba sasa mwili wako umeshachoka na hivyo unahitaji kupumzika. Yaani pale unapoona kwamba macho yanaanza kufunga,basi acha kufanya unachokifanya, nenda kalale.Mbinu itolewayo katika hili ni kusoma kitabu,gazeti nk.Ukiona kwamba unaanza kuruka kurasa au kuruka maandishi kwa sababu ya uchovu,jua kwamba umeshachoka na hivyo unatakiwa kwenda kulala.