Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 9:37 am

UMOJA WA ULAYA INADAI HAKUNA UWEZEKANO WA KUJADILI UPYA MAKUBALIANO YA NYUKLIA IRAN

EU: Hakuna uwezekano wa kujadiliwa upya makubaliano ya nyuklia ya Iran

EU: Hakuna uwezekano wa kujadiliwa upya makubaliano ya nyuklia ya Iran

Afisa mwandamizi wa taasisi moja ya Umoja wa Ulaya amesema hakuna uwezekano wala mpango wowote wa kuyajadili upya makubaliano ya nyuklia ya Iran.

Helga Schmid, Katibu Mkuu wa taasisi hiyo ya EU inayofahamika kama European External Action Service (EEAS) amesema Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) umethibitisha mara tisa kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana na Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kwa msingi huo, hakuna uwezekano wowote wa mapatano hayo kuangaliwa upya.

Schmid amesema hayo leo Jumanne katika mji wa Esfahan, katikati mwa Iran na kuongeza kuwa, wakuu wa EU katika kikao chao cha hivi karibuni walisisitizia haja ya pande zote kuheshimu na kutekeleza ipasavyo makubaliano hayo.

Makubaliano ya nyuklia ya Iran yalianza kutekelezwa Januari mwaka jana 2016

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel pamoja na wenzake wa Uingereza na Ufaransa, Boris Johnson na Jean-Yves Le Drian, walisisitiza kuwa, kulindwa mapatano ya nyuklia kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran ni kwa manufaa ya pande zote.

Kadhalika Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amekuwa akisisitiza kuwa, EU iko pamoja katika kulinda na kutetea makubaliano ya JCPOA na kwamba Ulaya ina maslahi ya kiusalama katika kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo na kushirikiana na Iran.

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akidai kuwa, makubaliano hayo ya JCPOA ndiyo mapatano mabaya zaidi katika historia ya Marekani na kwamba atashinikiza yaangaliwe upya au Washington ijiondoe kwayo.