Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:45 pm

SPORTS NEWS: MASHINDANO YA MCHEZO WA DRAFT YATIMUA VUMBI DODOMA

DODOMA: Katika kuendelea kuibua vipaji vya michezo wachezaji wa mchezo wa draft kutoka vilabu mbalimbali mkoani Dodoma wameanza kushiriki ligi ya mashindano ya Draft ambapo wadau wa mchezo huo wametakiwa kuendelea kuibua vipaji ili kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Mashindano hayo yanayoshirikisha jumla ya vilabu 12 vya mchezo wa draft kutoka manispaa ya Dodoma yameandiliwa na mbunge wa jimbo la Dodoma mjini Antony Mavunde huku lengo kuu ikiwa ni kukutanisha wadau wa mchezo huo na kuleta mwamko kwa jamii kushiriki mchezo huo

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo mkuu wa wilaya ya Dodoma Cristina Mndeme amesema mchezo wa draft ni miongoni mwa michezo inayopendwa ambapo amewataka wachezaji hao kuungana kwa pamoja na kuutangaza mchezo huo.

Kwa upande wake katibu mkuu wa umoja wa wachezaji wa draft Dodoma Tegemeo Saambili amesema kuwa lengo kuu ni kukuza mchezo wa draft na kuutambulisha mchezo huo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Baadhi ya wachezaji wa draft mkoa wa Dodoma akiwemo mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini mkoani Iringa Mohamed Mgimwa wamesema kuwa ili kuinua mchezo huo kuna kila sababu ya kuundwa mikakati ya kuibua vipaji vitakavyoweza kuutangaza mchezo huo.

Mashindano hayo yanatarajiwa kumalizika Oktoba 30 mwaka huu ambapo timu zinazoshiriki ni Eleven Stars,Chadulu,Bokoharamu,Chabela Camp,Kikuyu,Nzuguni,Mambo Poa,Chamwino,Ipagala,KDC,Area A na Iringa Road