Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 4:43 am

NEWS:WAZIRI MWAKYEMBE APANGUA KAULI YA RC MAKONDA.


Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema Taasisi ya Sanaa Bagamoyo (TaSUba) ni kiwanda cha wasanii na kushauri watu kuacha kukibeza.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo jana alipokuwa akifungua tamasha la 37 la sanaa na utamaduni Bagamoyo linalotarajia kufikia kilele Oktoba 27.

Kauli hiyo ya Mwakyembe inakuja ikiwa ni siku chache tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa katika hafla ya msanii wa muziki wa kizazi kipya Diamond (Nasiib Abdul) ya kukutana na wakazi wa Tandale kudai kwamba chuo hicho hajawahi kusikia kimetoa msanii maarufu.

Mwakyembe alisema historia ya chuo hicho inaonyesha wasanii wengi waliopikwa hapo wanafanya vizuri ikiwamo nje ya nchi na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia.

"Wanaofikiri chuo hiki hakina umuhimu watakuwa wanajidanganya sana, kwani hata hao maofisa sanaa na utamaduni mnaowaona nchi nzima asilimia 95 wametoka hapa na wamekuwa wakiisaidia Serikali kwa kiasi kikubwa.”

"Pia watendaji akiwamo Katibu wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo ambaye amewahi kushinda tuzo mbalimbali za filamu kimataifa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza ambaye ni mpigaji mzuri wa vyombo vya muziki wametoka hapa,” alisema na kuongeza:

"Bado tuna wahadhiri wengi katika vyuo vyetu vikuu ambao wamewapika wasanii wengine, sijui hao supastaa mnaowataka nyie ni wapi?" alihoji Mwakyembe.

Alishauri watu kwenda kupata historia ya chuo hicho kabla ya kukinyooshea kidole na utendaji wake na viongozi wa chuo nao kujitahidi kukitangaza ili kuepuka kuwapa watu nafasi kukizungumzia ndivyo sivyo.

Akizungumza kuhusu tamasha hilo la utamaduni linalokutanisha nchi 10 zikiwamo za Ulaya, Mwakyembe aliwasihi Watanzania kuhudhuria kwa wingi ili kujifunza tamaduni za watu mbalimbali.

Aliwataka wasanii kutumia fursa za warsha zinazotolewa katika kipindi chote cha tamasha hilo kama njia ya kuwasaidia kuboresha kazi zao.