Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:34 am

NEWS:DC MTATURU APEWA BARAKA NA WAZEE IKUNGI.

IKUNGI SINGIDA: Wazee wa wilaya ya Ikungi wamefanya shughuli ya kimila na kumpongeza mkuu wa wilaya hiyo Miraji Mtaturu kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia maendeleo kwa wananchi.


Akisoma risala kwa niaba ya wazee zaidi ya 130 waliohudhuria, mzee Rashid Msaru amesema kwa muda wa miaka miwili na nusu sasa tangu ateuliwe walikuwa wakifuatilia utendaji kazi wake kimya kimya na kuridhishwa nao.


“Kuna misemo ya Kiswahili imekuwa ikitumiwa na watanzania katika kuelezea jambo zuri au lililofanyika vizuri ambayo ni nyota njema huonekana asubuhi,au kizuri chajiuza kibaya chajitembeza,sisi wazee tumekuwa tukiona jitihada hizi na wala haihitaji elimu ya chuo kikuu kubaini utendaji kazi huu,”alisema mzee huyo.


Ametaja baadhi ya mambo aliyoyafanya katika kipindi hicho kuwa ni kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,usimamizi wa masuala ya ulinzi na usalama,usimamizi wa ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha shughuli za uchimbaji wa madini.


Aidha amesema kazi nyingine ni kusimamia na kutetea haki za wananchi wanyonge kama ilivyo dhamira ya Rais Magufuli,juhudi za kuwaunganisha wananchi pamoja bila ya kujali itikadi za vyama vyao na kuhakikisha sisi wazee tunatibiwa bure kwa kupewa vitambulisho maalum vya kututambua kama ilivyo dhamira ya serikali hii.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya,kijana wetu hatujakupongeza hivi hivi tu bali ni kutokana na juhudi zako,tunaomba pongezi hizi zisikamilishe ule usemi wa Kiswahili usemao mgema akisifiwa tembo hulitia maji bali ziwe chachu ya bidii ya kazi zako kwa ajili ya wana Ikungi,”aliongeza mzee huyo.


Akizungumza katika kikao hicho mkuu wa wilaya Mtaturu amewashukuru wazee hao kwa heshima waliyompa kwa kuandaa hafla ya kumpongeza na kuwaomba waendelee kumuunga mkono.

“Nimshukuru sana Rais wetu kwa kuniamini na kuniteua kuhudumu katika nafasi hii,mafanikio haya mnayonipongeza leo yametokana na ushirikiano wenu kwangu,ombi langu kwenu wazee wangu muendelee kuiunga mkono serikali kupitia sisi viongozi ili dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo iweze kufikiwa,”alisema Mtaturu.

Amesema serikali imeendelea kuimarisha huduma za elimu,afya,miundombinu,ulinzi na usalama na tayari wilaya imepokea pesa za elimu bure shilingi milioni 960 kwa mwaka mzima unaoisha sasa.

“Serikali inaboresha vituo viwili vya afya na tayari tumepokea shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya miundo mbinu ya afya,upande wa maji tumeshapokea shilingi milioni 761 na mchakato wa kupata wakandarasi wa kutekeleza miradi ya maji kwa vijiji vitatu vya Mwaru,Mtunduru na Ighuka unaendelea,”aliongeza kiongozi huyo.

Amesema wamepewa kibali cha kuchimba visima kwenye vijiji 20 lengo likiwa ni kufikia asilimia 75 ya utoaji wa maji kwenye wilaya kufikia mwaka 2020 na sasa wananchi wanapata maji safi na salama kwa asilimia 39.

“Namshukuru Rais wetu kwa kutuletea fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo milioni 49 za kutengeneza barabara za mitaa kwenye mji wa Ikungi ambapo mkandarasi ameshapatikana na ataanza kazi mapema mwezi Januari 2019.