Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 8:55 pm

NEWSA: MAGUFULI AAGIZA KUFUNGIWA KWA BENKI NA MAKAMPUNI YA SIMU.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, ameagiza mamlaka husika kuzichukulia hatua ikiwamo kuzifungia kampuni za simu na benki ambazo zitashindwa kuanza kutumia mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki ifikapo mwisho wa mwaka huu 2017.


“Kwa kampuni za simu au benki zitakazoshindwa kutekeleza agizo hili, taratibu husika zifanyike. Ikiwezekana makampuni hayo au benki hizo zifungiwe kufanya kazi nchini” amesema Rais Magufuli.


Rais Magufuli ameyasema hayo leo mjini Dodoma katika hafla ya ufunguzi wa tawi la benki ya CRDB lililopo katika jengo la LAPF-Dodoma.


Rais amezitaka benki zote pamoja na makampuni ya simu ambayo yanataka kuendelea kufanya biashara hapa nchini kuhakikisha kuwa wanajiunga na mfumo huu wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki kabla ya kufika mwisho wa mwaka huu wa 2017.


“Kwa taarifa nilizo nazo ni benki chache tu ambazo tayari zimejiunga na mfumo huu wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki. Benki na kampuni nyingi za simu bado hazijajiunga na mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki. Benki na Kampuni zote za simu zinazotaka kufanya biashara Tanzania zihakikihshe zinajiunga na mfumo huu kabla ya mwaka huu (2017) kuisha,” amesema Rais Magufuli.


Aidha Rais Magufuli ameagiza fedha kiasi cha shilingi 100 milioni alichopewa kama zawadi na Benki ya CRDB zitumike kujenga wodi ya wagonjwa katika hospitali ya Dodoma na kutaka wodi hiyo iitwe ‘wodi ya CRDB’ kama ishara ya heshima kwa benki hiyo.


Akiikabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rais Magufuli ameonya wahusika wote kutumia vizuri fedha hizo ili kuhakikisha ujenzi wa wodi hiyo unakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachofaa.