Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 8:51 am

NEWS: ZITTO NA MBOWE WAUNGANA UCHAGUZI WA MARUDIO

Kakonko: Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema na ACT-Wazalendo kwa pamoja vimeamua kusimamisha mgombea mmoja katika jimbo hilo atakayeungwa mkono na vyama vyote.

Katika makubaliano hayo, ACT- Wazalendo imeiachia Chadema Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, huku chama hicho kikuu cha upinzani kikiiachia ACT-Wazalendo Kata ya Gehandu iliyopo Hanang’ mkoani Manyara.

Makubaliano hayo yamefikiwa jana baada ya kumalizika kwa vikao ikiwa ni utekelezaji wa ushirikiano baina ya vyama uliotangazwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Wawili hao, ambao wakati fulani walionekana kuwa mahasimu ndani ya Chadema, walionyesha nia hiyo walipozungumza na waombolezaji waliojitokeza katika Uwanja wa Mwenge kumuaga aliyekuwa mbunge wa Buyungu (Chadema), marehemu Kasuku Bilago.

Makubaliano ya jana yalisainiwa na mkurugenzi wa uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi na mwenyekiti wa kampeni na uchaguzi wa ACT- Wazalendo, Mohamed Babu.

Mbali ya kuachiana jimbo la Buyungu na Kata ya Gehandu, vyama hivyo vilikubaliana kuungana mkono katika kata ambazo chama kimojawapo kitakuwa kimegombea na kushirikiana kukabiliana na hujuma katika kampeni, upigaji kura na utangazaji matokeo.

Taarifa ya pamoja ya vyama hivyo inasema Chadema itaiunga mkono ACT-Wazalendo kwenye kata ambazo ACT pekee imegombea na ACT Wazalendo itaiunga mkono Chadema kwenye kata ambazo Chadema pekee imeweka mgombea.

Pia inasema wagombea wa vyama vyote kwenye kata nyingine wataruhusiwa kuendelea na kampeni na ACT-Wazalendo na Chadema zitashirikiana kukabiliana na hujuma kwenye kampeni, upigaji kura na utangazaji wa matokeo.

Uchaguzi huo wa Agosti 12, unafanyika katika jimbo hilo baada ya Bilago kufariki akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akitibiwa.

Pia unafanyika katika Kata 77 huku CCM ikiwa imeshajikusanyia kata 30.

Vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo ni AAFP, CUF, DP, Demokrasia Makini, NRA, UMD na UPDP.

Chanzo mwananchi