Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:40 am

NEWS: ZITTO AHOJI SEREKALI KUTOTEKELEZA SHERIA KWA KUTOPELEKA SH TRIL 1.029 BENKI KUU

Dodoma: Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo Zitto Zuberi Kabwe amesema mpaka sasa Serikali haijazipeleka pesa Kiasi cha Sh1.029 trilioni ambazo zinazohitajika kuingia kwenye akaunti maalumu ijulikanayo kama Revenue Holding Account iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Mapato yote yanayokusanywa na Shirika la TPDC na kodi ya mapato inayokusanywa na TRA yanaelekezwa na sheria kwenda kwenye akaunti maalumu Benki Kuu inaitwa Revenue Holding Account. Sheria hiyo ( Oil and Gas Revenue Management Act No. 22 ya 2015) kifungu cha 8 inaanzisha mfuko huo maalumu,” amesema Zitto

Akizungumza Jana Jumatano Octoba 24, 2018 jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa ukuzaji wa viwanda katika sekta ya madini na uziduaji katika wiki ya asasi za kiraia inayoendelea jijini humo Zitto amesema tatizo kubwa ni kutotekelezwa kwa sheria zinazotungwa na Bunge na kwamba mwaka 2015 Bunge lilitunga sheria ya kusimamia fedha za mapato ya mafuta na gesi.

Amesema sheria hiyo imeelekeza kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 fedha zote ziende kwenye mfuko huo lakini tangu mwaka huo hakuna senti iliyokwenda.

Kongamano hilo limeandaliwa na asasi nane za kiraia ikiwemo Foundation for Civil Society, Policy Forum, Haki Raslimali, CBM, Taasisi ya Wajibu, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Nchini (THRDC), Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata).