Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 5:57 am

NEWS: WAZIRI MKUU AMUAGIZA RC DODOMA KUKAGUA UBADHIRIFU WA BIL 1.2


Dodoma: Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahengeampeleke na Afisa Kilimo wa mkoa Bw. Bernad Abraham wakakague mradi wa umwagiliaji wa Mpwayungu wilayani Chamwino ili kubaini waliohusika na ubadhilifu wa sh. bilioni 1.2 za mradi huo.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana jioni (Jumamosi, Oktoba 20, 2018) baada ya mbunge wa jimbo Mtera, Livingstone Lusinde kumuomba awasaidie kuhusu upotevu wa sh. bilioni 1.2 zilizotolewa kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji ambazo matumizi yake hayajulikani.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi wilayani Chamwino, Dodoma alipokea ombi hilo la mbunge wakati akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Mpwayungu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mpwayungu.

Alisema mara baada ya Afisa Kilimo, Bw. Abraham kukamilisha ukaguzi wa mradi huo wa umwagiliaji apelekewe taarifa ili waliohusika na ubadhilifu wa kiasi hicho cha fedha wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alivunja kamati ya kusimamia huduma maji ya kijiji cha Mpwayungu na alimuagiza Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Chamwino Bw. Godfrey Mbabaye aunde kamati mpya.