- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: WAZIRI MKUU AMKABIDHI WAZIRI JAFO ORODHA YA WATUMISHI.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI, Selemani Jafo orodha ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ili awachukulie hatua baada ya kugoma kuhamia katika kituo chao cha kazi na kuendelea kuishi jijini Dodoma.
Amemkabidhi orodha hiyo jana (Ijumaa, Oktoba 19, 2018) baada ya mkuu wa wilaya hiyo Bibi Mwanahamisi Mukunda kusoma taarifa ya wilaya, ambayo pamoja na mambo mengine alieleza kuwa watumishi wote wameshamia kwenye kituo chao cha kazi na wanaishi. Waziri Mkuu alikuwa katika kikao na Watumishi wa Halmashuri hiyo.
“Mkuu wa wilaya umedanganywa watumishi bado wanaishi jijini Dodoma, walichokifanya baadhi wamejiunga watatu na wamekodi chumba kimoja. Namkabidhi Waziri wa TAMISEMI orodha ya watumishi hawa ambao wamegoma kuishi kwenye kituo chao cha kazi ili uwashughulikie”
Waziri Mkuu amesema watumishi hao wamegoma kuhamia katika kituo chao cha kazi licha ya Serikali kuwataka kufanya hivyo.”Maelekezo hatuyatoi kwa ajili ya kujifurahisha, bali tunataka utekelezaji ufanyike ili wananchi waweze kuhudumiwa ipasavyo.”
Jumatano, Juni 27, mwaka huu, Waziri Mkuu wakati akizinduavituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura wilayani Bahi, aliwaagiza watumishi wa Halmashauri hiyo wanaoishi nje ya kituo chao cha kazi wahamie kituoni kwao.
Waziri Mkuu alisema Serikali inataka watumishi wa umma wawajibike na waishi katika vituo vyao vya kazi. “Nawataka watumishi wote wa wilaya hii wanaoishi jijini Dodoma wawe wamehamia hapa ifikapo Julai 30 mwaka huu na wasiohamia nipewe majina yao.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Bahi wakiwemo madiwani na wakuu wa idara wahakikishe wanamaliza tofauti zao na washirikiane katika kufanyakazi kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi.
Awali, Waziri Mkuu alikagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya sekondari ya Mpalanga yenye uwezo wa kukaliwa na walimu sita, ambapo amesema ameridhishwa na ujenzi huo. Mradi huo unagharimu zaidi ya sh. milioni 140.
Pia Waziri Mkuu amezindua daraja la Chipanga ambalo ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 2.18 na kisha alitembelea kituo cha Afya cha Bahi ambako alikagua wodi ya wazazi na kuzungumza na akinamama ambao waliishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya.