Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 5:37 am

NEWS: WAZIRI MHAGAMA AWATAKA WADAU WANAOANDAA MWONGOZO KUHAKIKISHA UNAKAMILIKA KABLA YA MWAKA HUU KUISHA.

DODOMA: Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi ajira, vijana, na watu wenye ulemavu Jenista Mhagama amewataka wadau mbalimbali wanaoshiriki katika mchakato wa uandaaji wa mwongozo wa kitaifa wa ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya kimkakati kuhakikisha unakamilika kabla ya mwaka huu kuisha.

Waziri Mhagama ameyasema hayo leo wakati akifungua warsha ya wadau hao iliyoandaliwa na taasisi ya uongozi kwa kushirikiana na baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC) inaliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema muongozo huo kukikamilika ndani ya mwaka huu utasaidia suala la uwezeshaji wa wananchi kukamilika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwa linahitaji jitihada za makusudi.

“Mwongozo huu umeeleza bayana kwamba Wizara na Taasisi za Serikali zihakikishe kwamba Sera, Sheria, Kanuni na mikataba wanayoingia inazingatia suala la ushiriki wa wananchi, hivyo taasisi zinatakiwa zitengeneze mfumo madhubuti wa kuweza kufuatilia na kuhakiki ushiriki wa watanzania katika miradi mbalimbali,” amesema Mhagama.

Hata hivyo Mhagama amesema mpango huo unaelekeza kabla ya miradi kuanza ni vyema mwekezaji au mkandarasi atengeneze mpango wa ushiriki wa watanzania ambao utaainisha mpango wa ajira, ununuzi, uongezaji ujuzi, uhamishaji wa teknolojia na ushiriki wa jamii inayozunguka eneo la uwekezaji.

Amesema kuwa Mipango hiyo ikiandaliwa mapema itawezesha nchi kuandaa nguvu kazi inayohitajika na kuwawezesha sekta binafsi kujua fursa zitakazopatikana katika mradi husika mapema ili kuweza kujipange vizuri.

“ Ni lazima kila sekta ifanye jitihada za makusudi ili kuhakikisha kwamba watanzania wanashiriki kikamilifu katika ajira kwenye ngazi zote na bidhaa na huduma za watanzania zenye ubora zinatumika. Kwa kufanya hivi itapunguza kwa kiwango kikubwa changamoto ya ajira hasa kwa vijana na itawezesha sekta binafsi ya kitanzania kukua” amesema.

Awali akizungumza mwenyekiti baraza la NEEC Dk, Festus Limbu amesema kuwa wanaimani kupitia mpango huo Tanzania itafikia uchumi wa kati kabla ya kufika mwaka 2025.

“Kwa jinsi tulivyojipanga vumbi litaanza kutimka kuanzia sasa ili kuwafanya watanzania kutokuwa watanzamaji katika miradi mbalimbali mikubwa ya kimaendeleo,” amesema.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika mafunzo hayo Mkuu wa idara ya Mafunzo kwa Viongozi wa taasisi ya uongozi Kadari Singo amesema kuwa wakati wa taifa kupata muongozo wa kuwaongoza watanzania kunufaika miradi inayotekelezwa nchini ni sasa.