Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:48 pm

NEWS: WAZIRI MBARAWA AWAFUTA KAZI WAKANDARASI 2

Dodoma: Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa amewatimua wakandarasi wawili waliokuwa na miradi mikubwa ya maji sehemu tofauti tofauti hapa nchini huku akisema kuwa wakandarasi wajinga na wahuni hawawezi kufanya nao kazi,

Prof Mbarawa amedai ya kuwa wakandarasi hao wamefilisika na hawana uwezo wa kuendesha miradi.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 15, 2018 Profesa Mbarawa amewataja waliotimuliwa kuwa ni Overseas Infrastructure Alliance (India) Pvt Ltd aliyekuwa na mkataba wa kujenga mradi wa maji na usafi wa mazingira Mjini Lindi.


Mwingine ni Spencon Service Ltd aliyekuwa anajenga mradi wa Maji Kigoma ambao wote kwa pamoja imeelezwa wamefilisika na hakuna uwezo tena.


Hata hivyo, katika hali ya kushangaza licha ya kuelezwa kuwa amefilisika lakini Overseas amerudishwa kuendelea na mradi wa maji wa Chalinze mkoani Pwani.

Waziri amesema wakandarasi hao kwa sasa hawawezi kupewa miradi mingine mahali popote kwani wameitia Serikali hasara kubwa na kuwapa usumbufu wananchi.


“Mkandarasi wa Lindi alipaswa kukamilisha mradi Machi 2015 lakini tukamuongezea muda hadi Desemba 2015 cha kushangaza hadi leo amefikia asilimia 92.3 tu akiwa amelipwa Sh27.925 bilioni kati Sh30.389 bilioni alizoingia mkataba,” amesema Mbarawa.


Kuhusu Mkandarasi wa Kigoma amesema mkataba wake ulikuwa sawa na mwenzake lakini hadi sasa amefikia asilimia 87 akiwa amelipwa ShSh 39 bilioni kati ya Sh42 bilioni walizoingia mkataba na Wizara.

Kuhusu miradi hiyo amesema itaendelea kutekelezwa chini ya wakandarasi wengine ambao Serikali itaingia nao mikataba na akazungumzia kuhusu kuvunjwa kwa mikataba kwamba haitakuwa na shida kwani wamejiridhisha maeneo yote.