Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 11:34 pm

NEWS: WAZIRI MBARAWA ATOA ONYO KWA MAMLAKA ZA MAJI KUACHA TABIA YA KUWABAMBIKIZIA BEI ZA ANKARA ZA MAJI WATEJA.

DODOMA: Waziri wa maji Prof. Makame Mbarawa, ametoa onyo kwa mamlaka za maji na usafi wa mazingira nchini kuacha tabia ya kuwabambikizia bei za ankara za maji wateja.

Aidha ametoa onyo kwa wakuu wa mamlaka hizo ambao bado wanatoza gharama za huduma kwa wateja (Services Charges) kuacha mara moja kwani atakaye bainika mshahara wake utakatwa ili kurejesha fedha za wateja.

Mbarawa ameyasema hayo leo wakati alipokua akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa watendaji wa mamlaka za maji za mikoa na wilaya kinachofanyika jijini hapa.

Amesema kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja kubambikiziwa ankara za maji na mamlaka za maji katika maeneo mbalimbali.

“Tusiwabambikizie wateja wetu bill za maji kiasi ambacho hawajatumia, wananchi wengi wamekuwa wakilalamika sana katika maeneo ambayo nimekuwa nikipita kuzungumza nao… hivyo niwaombe watendaji wote kuacha mara moja tabia hii”amesema Prof. Mbarawa.

Akizungumzia juu ya malipo ya gharama za huduma amezitaka mamlaka zote za maji nchini kuacha kutoza wanachi na atakae bainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

“Services Charge tulishaziondoa lakini bado nasikia katika baadhi ya mamlaka watu bado wanatozwa fedha hizi ambazo tulikubaliana kwa pamoja kuziondoa sasa atakaye bainika hivi sasa kuwa bado anaendelea kutoza wanachi mshahara wake utakatwa ili kufidia kiasi ambacho wateja wamelipa”amesema.

Prof. Mbarawa pia ameziagiza mamlaka zote za maji nchini kuongeza udhibiti wa maeneo yanayotumika kutibu maji kwa kuweka ulinzi ikiwemo kufungwa mifumo ya kielekitroniki.

“Jambo hili naomba mlifanye haraka sana bila kuchelewa uwepo ulinzi wa askari pamoja na mifumo ya cctv camera ili hata kama likiharibika lolote tunakwenda kurejea katika video na kuona nini kilitokea…eneo la kutibu maji ni eneo nyeti sana leo hii ukienda nchi kama Misri kuingia katika eneo hili lazima uwe na kibari maalum”amefafanua Prof. Mbarawa.

Aidha ameitaka mamlaka ya udhibiti wa maji na nisahti kwa kushirikiana na wizara kuona namna gani ambavyo wanaweza kuweka utaratibu wa bei moja kwa huduma ya maji vijijini.

“Leo hii ukienda vijiji unakuta baadhi ya maeneo ndoo ya lita 20 wananunua kwa sh. 500, wengine 200 na wengine 100 hivyo lazima tuwe na bei ambayo itafahamika kwa kila eneo”alisema

Hata hivyo ametoa onyo kwa mamlaka ambazo zimekuwa na tabia ya kushindwa kulipa ankara za umeme pamoja na madawa ya kutibu maji.

“Katika utawala wangu mimi kama waziri wa maji sitakubaliana na mamlaka ambazo zimekuwa zikishindwa kulipa umeme na kutaka wizara iwalipie kutoka katika mfuko wa maji wakati wanatoa huduma na wanalipwa”amesema

Katika kikao hicho Prof. Mbarawa alisema wizara hiyo itaweka mfumo wa kuwapima wakuu wa mamlaka za maji kwa kila baada ya miezi mitatu na atakayeshidwa ataondolewa katika nafasi yake.