Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 8:33 am

NEWS: WASICHANA 10 BORA WAIBUKA KIDEDEA UFAULU KIDATO CHA II

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa kwa wanafunzi wa kidato cha pili na darasa la nne huku wasichana waking’ara.

Kwa upande wa kidato cha pili, wasichana wameshika nafasi zote 10 bora kutoka kwenye shule tatu za Feza Girls, Canossa na Precious Blood. Kwa darasa la nne, wasichana wameshika nafasi nane za juu na wavulana wakishika nafasi ya tisa na 10. Katika matokeo ya mwaka 2016, wasichana walikuwa wanane na wawili wavulana, na mwaka 2015 wavulana walikuwa watano na wasichana watano.

Akizungumzia matokeo ya kidato cha pili, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema wanafunzi 433,453 ambao ni asilimia 89.32 wamepata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuendelea na Kidato cha Tatu. Kati ya hayo wasichana ni 224,736 ambao ni asilimia 88.55 na wavulana ni 208,717 ambao ni asilimia 90.17.

Aidha, Msonde alisema wanafunzi 51.807 ambao ni asilimia 10.68 wamefeli kwa kushindwa kupata alama za kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu. Mwaka 2016 wanafunzi 372,228 (asilimia 9.02) waliendelea na kidato cha tatu huku wanafunzi huku asilimia 8.98 ambao ni wanafunzi 36,737 walifeli.

Mwaka 2015, ufaulu ulikuwa ni asilimia 89.12 ambao ni wanafunzi 324,068 huku wanafunzi 39,567 ambao ni asilimia 10.88 walifeli mtihani huo. Msonde alisema ufaulu katika masomo ya msingi ya Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Fizikia, Kemia, Hisabati umepanda huku ufaulu wa masomo ya Civics, Historia na Biolojia umeshuka, ukilinganisha na mwaka 2016.

“Somo ambalo wanafunzi wamefaulu zaidi ni Kiswahili kwa asilimia 91.92 na lile la ufaulu wa chini ni Hisabati yenye asilimia 32,” alisema. Akizitaja shule 10 zilizofanya vizuri kuwa ni Kemebos (Kagera), Canossa (Dar), St. Francis Girls (Mbeya), Marian Boys (Pwani), Kilimanjaro Islamic na Precious Blood (Arusha), St Augustine-Tagaste (Dar), Don Bosco Seminary (Iringa), Marian Girls (Pwani na Anwarite Girls (Kilimanjaro).

Shule 10 za mwisho ni Malegesi (Mtwara), Ukata (Ruvuma) Mswaha na Mlungui (Tanga), Madangwa (Lindi), Mayo Day (Tanga), Lengo (Mtwara), Kwemashai, Mbwei na Zirai (Tanga). Akitaja wanafunzi 10 bora kitaifa ni Shamimu Mohamed na Rukia Abdallah (Feza Girls), Jacqueline Kivuyo, Maina Kashumba, Kate Mgabo, Sylvia Tibenda, Zuhura Sapi na Gladys Maluli (Canossa).