Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 3:50 am

NEWS: WALIOTENGENEZA MIFUKO FEKI YA SUKARI KUNYANGANYWA LESENI

Dodoma: Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amemuagiza Mkurugenzi wa Viwanda Nchini kuwanyang’anya leseni wamiliki wa viwanda wote waliothibitika kutengeneza mifuko ya sukari bandia.

Amesema watu waliotengeneza mifuko hiyo na wale walioweka sukari wote wana hatia kwa sababu walitakiwa kuweka taarifa zote katika label ya mfuko kama sheria za ushindani na ubora wa bidhaa zinavyowataka.

Akizungumza leo Oktoba 24 ofisini kwake, Mwijage amesema kuwa hivi karibuni kumeibuka watu wanaotengeneza mifuko halafu wanaweka sukari kinyume na taratibu na sheria za nchi.

“Mtu yeyote ambaye amehusika kutengeneza mifuko ya chakula ajisalimishe FCC (Tume ya Ushindani Nchini) na wizarani kusudi tuone kama tunaweza kumsimamia akaendelea kuzalisha,”amesema.

“Jambo lililotokea hivi karibuni kuna watu wanatengeneza mifuko halafu hiyo mifuko wanaweka sukari sasa nichukue nafasi hii kuwaelimisha wenzangu ambao tunashirikiana sote wasiwe na kigugumizi katika hili,”amesema.

“Kwa sababu wizara yangu ndiyo inasimamia suala la FCC, mtengenezaji wa mifuko ya kuweka bidhaa kwa mfano uko Tanzania una kiwanda ukatengeneza mifuko unaandika made in Brazili na uko Tanzania ni kosa.”

Pia Waziri amezitaka taasisi zote za Serikali kusaidiana na kuzungumza nyimbo moja na kwamba aliyekiuka maelekezo hayo lazima aende kwenye vyombo vya sheria. Aliwataka watakaoshindwa kwenda kutafsiri hizo sheria wamrudie yeye.