- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: WAKULIMA WA KOROSHO WAWEKA KAMBI KWA MKUU WA WILAYA KWASAA 7
Wakulima wa korosho,na wenyeviti wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) wilayani Masasi, jana waliweka kambi kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Selemani Mzee kwa zaidi ya saa saba wakishinikiza serikali kulipa fedha zao za korosho wanazodai.
wakuilma hao waliona ni busara kuchukua hatua hiyo kutokana na serikali kutowalipa fedha za korosho, huku baadhi yao wakidai kuwa walipewa ahadi ya kufanyika ukaguzi wa mashamba yao baada ya kubainika korosho walizouza ni zaidi ya kilo 1,500.
Taratibu za malipo kwa walikuma wa zao hilo zinataka mkulima yeyote mwenye kilo zaidi ya 1,500 lazima akaguliwe shamba lake kabla ya malipo kufanyika.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, (Mzee) aliamua kufanya kikao maalum cha dharura na wakulima hao akiwa na wajumbe wengine wa Kamati yake ya Ulinzi na Usalama na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Masasi, Eduward Mmavele, ili kwa pamoja kusikiliza malalamiko ya wakulima hao.
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa Wilaya, mmoja wa wakulima hao ambaye ameuza korosho zake kwenye Chama cha Msingi Tuaminiane (AMCOS), Saidi Khatau, alisema ni miongoni mwa wakulima wanaotakiwa kufanyiwa ukaguzi wa mashamba yao. Alisema wanashangaa kuona ahadi ya serikali ya kukagua mashamba yao haitekelezwi licha ya kuuza korosho.
Alisema wakulima hawajui ni lini serikali itawalipa fedha zao na hawafahamu lini jopo linalofanya ukaguzi wa mashamba ya wakulima litafika shambani kwake, ili aingizwe kwenye orodha ya majina ya wakulima ambao watalipwa fedha zao.
Mkulima mmoja wa korosho, Jacob Hokororo, alidai kuuza kilo 1,563 za korosho kwa chama cha Tuaminiane, alidai kuna kundi kubwa la wakulima hajalipwa fedha za mauzo ya zao hilo.
Alisema haoni haja kwa sasa serikali kutumia muda mwingi kukagua mashamba ya korosho kwa kuwa zipo takwimu za miaka ya nyuma kuhusu ukaguzi wa mashamba hayo. Everina Kambulage, mkulima aliyeuza kilo 470 za korosho, alisema kiwango alichouza hakihitaji ukaguzi wa shamba lake, lakini hajalipwa hata senti moja.
Alisema anaiomba serikali kuharakisha mchakato wa wakulima, hasa wenye kiwango kidogo cha korosho, kulipwa fedha zao.
Alisema hali ya wakulima ambao hadi sasa hawajalipwa fedha zao ni mbaya, akidai wanashindwa kuendesha maisha yao kutokana na kukosa fedha.
Kiongozi wa Chama cha Msingi Lulindi AMCOS, Shiraji Athuman, alisema wamepata faraja kukutana na Mkuu wa Wilaya kwa kuwa chama chao ni miongoni mwa vyama ambavyo wakulima bado hawajalipwa fedha zao na hawajaelezwa sababu za kutofanyika kwa malipo hayo.
“Sisi viongozi wa AMCOS kwa sasa tunashindwa kuishi vizuri na familia zetu huko vijijini kwa sababu ya wakulima kutolipwa fedha zao, wanahitaji kufahamu kwanini serikali bado haijawalipa fedha zao hadi sasa na kila siku wanasikia serikali ikisema wakulima wamelipwa. Kwa kweli usalama wa maisha yetu ni mdogo, tunaomba kulipwa," alisema.
Akijibu maombi yao, Mkuu wa Wilaya ya Masasi (Mzee) alisema amesikiliza kwa umakini malalamiko ya wakulima na akasisitiza serikali bado inaendelea kuwalipa wakulima, hivyo kuwataka wawe wavumilivu.
“Nawaomba muwe wavumilivu kwa kuwa kila mkulima ambaye ni mkulima halali, lazima atalipwa fedha zake," alisema.
"Kuhusu suala la ukaguzi wa mashamba, hili nitakaa na wahusika kujua tatizo liko wapi, lakini ni lazima serikali inawalipa wakulima kupitia taratibu zake ambazo zinalenga kuhakikisha anayelipwa ni mkulima halali."