Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 11:46 pm

NEWS: WAISHI NJE BAADA YA NYUMBA ZAO KUCHOMWA NA MOTO

MANYARA: Wakazi wa kijiji cha Manyara kata ya Magara eneo la kambi ya fisi wilayani Babati mkoani Manyara wamejikuta wakilala katika mahema baada ya makazi yao kuchomwa moto na Kubomolewa na serikali kwa maelezo kuwa maeneo wanayoishi ni ya hifadhi ya ziwa Manyara.



Kituo hiki kilifika katika kijiji hicho ambacho kipo pembezoni mwa ziwa Manyara na kukuta majivu ambapo nyumba 86 zimeteketezwa kwa moto na kubomolewa.


Wakizungumza na kituo hiki wanakijiji hao walieleza kuwa hawajui kwanini wamebolewa nyumba zao ili hali wameanza kuishi tangu miaka ya 1984,zaidi ya miaka 30 sasa.


Baadhi yao wamesema hawakuwepo wakati zoezi hilo la kuchoma na kubomoa nyumba likiendelea wamekuta vitu vyao vikiwa nje huku badhi vikiwa vimeteketea kabisa.


Akielezea Mgogoro huo kati ya kijiji na Halmashauri ya wilaya Mwenyekiti wa kitongoji hicho Wiliam Muna amesema kuwa mgogoro huo umeanza tangu mwaka 2013.


‘’Alama za mpaka wa kijiji ziliwekwa mwaka 2003 baada ya hapo pakawa na marekebisho ambapo wananchi walipewa maeneo haya na kukabidhiwa risiti na Halmashauri ya kijiji’ alisema Muna.


Muna alisema ‘’Mimi kama kiongozi wa kitongoji jambo hii imeniumiza sana kwani wananchi wamekosa haki zao,na hata fidia hawakupatiwa.’’


Aliendelea kusema kuwa Maeneo hayo yamechukuliwa na mwekezaji kutoka Jumuiya ya uhifadhi wanyamapori [Juibu].


Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Hamisi Iddy Malinga alifika katika eneo hilo na kueleza kuwa wameamua kuwaondoa kwa nguvu wananchi hao kwa kuwa wamefanya hivyo kuwaondoa ili kuendelea kulilinda ziwa Manyara.


Suala ambalo limejitokeza kwenye ekolojia wa Tarangire Manyara ni uharibifu wa Ziwa Manyara lakini pia ushoroba unaounganisha Tarangire-Manyara.


Malinga amesema Katika eneo la kijiji cha Manyara kumekuwa na vijiji kadhaa ambavyo siku ya nyuma waliingia mpaka kwenye maeneo ya uhifadhi [eneo la kijani] lakini baada ya serikali kuwatangazaia waliondoka lakini imekuwa vigumu kijiji cha Mnayara kutii agizo hilo.


Mpaka sasa wanakijiji hao wamejikusanya kwa majirani wakiwa na watoto wao huku kukiwa na hofu ya kupata magonjwa ya milipuko kama vile kipindu pindu na kuhara kwani hakuna vyoo hali inayowalazimu kujisaidia vichakani.