Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 2:42 am

NEWS: WABUNGE WA CHADEMA WAPITISHWA NA CCM KUGOMBEA UBUNGE

Dar es Salaam: Chama cha mapinduzi CCM kimewapitisha waliokuwa wabunge wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho kikongwe nchini.

Maamuzi hayo yamefanyika kupitia Kamati Kuu ya chama hicho kilichokutana leo Jumanne Oktoba 30, 2018 katika ofisi ndogo za umumba jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais John Magufuli.

Chama hicho kimewapitisha wagombea hao ambao watashiriki uchaguzi mdogo utakaofanyika Desemba 2, 2018.

Waliopitishwa kugombea ni Pauline Gekul (Babati Mjini), James Millya (Simanjiro), Joseph Mkundi (Ukerewe) na Marwa Chacha wa Serengeti.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 30, 2018 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole mbali na kueleza kupitishwa kwa wagombea hao, pia imebainisha kuwa Desemba 15, 2018 ndio itakuwa mwisho wa kupokea maombi ya uanachama wa CCM na kupewa dhamana ya uwakilishi kupitia tiketi ya CCM kwa wabunge na madiwani kutoka vyama vingine.

“Ieleweke kwamba baada ya tarehe hii wabunge na madiwani watakao omba kujiunga na CCM watapokelewa na kubaki kuwa wanachama wa kawaida,” inaeleza.

“Zoezi la uandikishwaji wa wanachama wapya linaendelea kwa mujibu wa taratibu za kawaida za chama huku zoezi hili likienda sambamba na usajili wa wanachama na maandalizi ya utolewaji wa kadi za kielektroniki za chama.”