Home | Terms & Conditions | Help

November 29, 2024, 6:42 am

NEWS: VIONGOZI WA SUDAN KUSINI WAGAWANA MADARAKA

Serikali na waasi nchini Sudan Kusini wametia mkataba wa kugawana madaraka, ili kumaliza vita vya karibu miaka minne ambavyo vimekuwa vikiendelea katika taifa hilo changa duniani.

Mkataba huo umetiwa saini jijini Khartoum nchini Sudan baada ya pande mbili kukubaliana, baada ya mazungumzo ya muda mrefu.

Kwa mujibu wa makubalino hayo, kiongozi wa waasi Riek Machar atarejea kama Makamu wa kwanza wa rais, katika serikali ya umoja wa kitaifa itakayoongozwa na rais Salva Kiir.

Aidha, imekubaliwa kuwa kutakuwa na mawaziri 35. Rais Kiir atakuwa na mawaziri 20 huku Machar akiwa na tisa huku wapinzani wengine wakigawana nafasi sita zinazosalia.

Pamoja na hilo, kutakuwa na wabunge 550. Upande wa rais Kiir umepewa wabunge 332 huku kundi la Machar likipata wabunge 128.

Baada ya mkataba huu kukubaliwa, rais Kiir na Machar sasa wanatarajiwa kutia saini mkataba wa mwisho hivi karibuni nchini Kenya na baada ya miezi mitatu, serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa itaundwa kuongoza nchi hiyo kwa miezi 36 kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu.