Home | Terms & Conditions | Help

November 28, 2024, 1:31 am

NEWS: UTATA WAENDELEA KUIBUKA SAKATA LA BALOZI UMOJA WA ULAYA

Taarifa za kufukuzwa kwa Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania huku taarifa nyingine inayodaiwa kutolewa na msemaji wa ubalozi wa EU jijini Dar es Salaam inasema, taarifa zinazodai kuwa Balozi Roeland Van amefukuzwa nchini hazina ukweli.

“Ukweli ni kwamba, Balozi Roeland Van ameitwa Makao Makuu (Brussels), nchini Ubelgiji, kwa ajili ya kushauriana juu ya siasa na uhusiano wa baadaye kati ya Jumuiya ya Ulaya na Tanzania,” imeeleza taarifa kupitia mitandao ya kijamii, inayodaiwa kutolewa na msemaji wa ubalozi huo.

Hata hivyo, taarifa inayodaiwa kutolewa na msemaji wa ubalozi haina jina la mtoaji wala anuani ya mahali ilikotolewa.

Aidha, taarifa kuwa Balozi Roeland Van ameitwa makao makuu kwa ajili ya kinachoitwa, “kuangaliwa upya uhusiano wa kati ya serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya,” haikueleza kwa undani sababu za kuitwa huko.

Vilevile, hata taarifa inayodaiwa kuwa ya serikali inayoeleza ya kufukuzwa kwa balozi huyo nchini, haikueleza sababu za kuchukua hatua hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Balozi Roeland Van anatakiwa kuondoka nchini kabla ya saa sita usiku wa tarehe 3 Novemba.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na waliobobea kwenye nyanja ya diplomasia ya kiuchumi wanasema, taarifa zote mbili – kufukuzwa ama kuitwa makao makuu kwa balozi – hazina afya njema kwa taifa.

“Hata kama ameitwa makao makuu, bado hiyo habari njema kwa Tanzania,” anaeleza Dk. Marccossy Albenia, mtafiti na mchambuzi wa masuala ya uchumi wa diplomasia.

Anasema, “ikiwa Ulaya wameona kuna mahusiano mabaya na Tanzania na hivyo wamemuondoa balozi wao nchini na kumtaka atoe maelezo ya hali halisi na akapate maelezo upya, hii ni hatua mbaya zaidi, kuliko kumfukuza.”

Anasema, “ni sharti serikali itafakari haraka mahusiano yake kidiplomasia. Siyo sifa kuwa mgomvi, ndio maana kuwa diplomasia, kwamba utatua changamoto zako kwa njia ya kujenga mahusiano mema.”

Naye mmoja wa aliyepata kuwa balozi wa Tanzania katika nchi za Ulaya, Marekani na Umoja wa Mataifa na ambaye baadaye akaja kuwa waziri katika serikali ya Benjamin Mkapa anasema, “..kama madai haya ni ya kweli, tunakoelekea kutakuwa ni kubaya sana.”